Michezo

Mabadiliko sheria tano za soka kutoka FIFA, kuchezwa dakika 60, kadi za njano na mengine

Shirikisho la mpira wa miguu ulimwenguni FIFA, lipo katika kufanya majaribio ya mabadiliko ya baadhi ya sheria ambazo huwenda zikaja kuanza kutumika siku za usoni huku lengo kuu ikiwa ni kuuboresha zaidi mchezo huo pendwa.

Majaribio hayo yameanza kufanywa kwenye Mashindano ya Vijana yanayoitwa ‘Future Of Football Cup’ ambapo SC Heerenveen, AZ Alkmaar, PSV Eindhoven na Club Brugge PSV, AZ Alkmaar, RB Leipzig na Club Brugge ni miongoni mwa timu za vijana ambazo zinashiriki kwenye mashindano hayo ya majaribio ya FIFA yanayo husu mabadiliko makubwa ya sheria.

Mabadiliko ya sheria tano (5) mpya katika mchezo huo wa soka yanakuja ambazo zinaweza baadaye kupendekezwa kuwa rasmi katika mashindano yote ya mpira wa mnguu.

Sheria hizo tano (5) mpya ambazo FIFA wanazifanyia majaribio katika mashindano hayo ya Future of Football Cup ni kama zifuatazo.

1. MECHI KUCHEZWA DAKIKA 60, BADALA YA 90.

Moja katiya sheria ambazo Shirikisho la Mpira wa Miguu duniani FIFA inazifanyia majaribio ni mpira kuchezwa dakika 60 badala ya 90 kama ilivyozoeleka.

Kwa maana hiyo kipindi cha kwanza kitakuwa na dakika 30, na kipindi cha pili mwamuzi atachezesha hizo hizo 30 na hatimaye kukamilika dakika 60 na sio dakika 90 tena.

Mwamuzi wa mchezo pia atasimamisha saa yake endapo kuna kitu chochote kitatokea uwanjani kama vile mabadiliko ya wachezaji, mpira kutoka nje nk.

2. IDADI YA WACHEZAJI WA ‘SUB’ KUONGEZEKA (substitution)

Kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Corona duniani, idadi ya mabadiliko ya wachezaji imeongezeka kutoka watatu (3) hadi kufikia watano (5).  FIFA inafanya majaribio katika mashindano hayo ya The Future of Football kuangalia kama itawezekana timu kufanya mabadiliko ya wachezaji kadri timu husika itakavyoweza.

3. KADI ZA NJANO

Maboresho yanayofanyika ni kuwa mchezaji anapopewa kadi za njano atatoka nje ya uwanja kwamaana ya kwenda benchi kwa muda wa dakika tano (5) kisha ataruhusiwa kurejea tena uwanjani.

Kwa mantiki hiyo kadi za njano zitakuwa na adhabu zaidi kuliko ilivyozoeleka kwa sasa.

4. MIPIRA YA KURUSHA

Inatarajiwa pia kuondoa sheria ya mipira ya kurusha, endapo mpira ukitoka nje utaanzwa kwa kuweka chini kisha kupigwa kwa miguu na sio kurushwa kama ilivyozoeleka hivi sasa.

5. CHENGA KWENYE KONA (Dribbling)

Mipira ya kona mchezaji ataruhusiwa kuanzisha mpira mwenyewe pasipo kupata msaada kutoka kwa mchezaji wa timu yako. Mchezaji anayepiga kona anaweza kupiga chenga mwenyewe bila kumuanzishia mchezaji mwenzake.

Mwanzoni mwa mwaka huu Florentino Perez alikuja na wazo la kupunguzwa kwa muda kwenye mchezo wa soka wakati walipokuwa wakiitengeneza michuano ya European Super League ambayo ilikuja kupigwa marufuku.

Alipozungumza na El Chiringuito, Perez alisema “Mpira lazima ubadilike, lazima tuchambue kwa nini vijana wenye umri kati ya 16 hadi 24 asilimia 40 miongoni mwao hawavutiwi na soka. Wanasema mechi huwa ndefu mno, na hivyo wanaingia kwenye ‘platforms’ nyingine za burudani. Ni lazima tubadilike kama tunahitaji mchezo wa soka uwendelee kuishi.”

Naye Bosi wa kitengo cha maendeleo ya soka ndani ya FIFA, Arsene Wenger aliwahi kusema siku zijazo sheria nyingi za soka zitabadika.

Je, unaungana na maboresho hayo ?

Imeandikwa na @fumo255  na Raheem Rajuu

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents