Majeshi SADC yatakiwa kushiriki mafunzo ya ulinzi wa amani

MAJESHI kutoka nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) yametakiwa kushiriki mafunzo mbalimbali yanayotolewa kuhusiana na masuala ya ulinzi wa amani ili kupata uelewa wa pamoja utakaowasaidia wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Rai hiyo imetolewa leo Machi 24, 2025 jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Juu ya Kijeshi Kunduchi, Meja Jenerali Suleiman Mzee wakati akifungua Kozi ya siku tano ya Uongozi kwa viongozi waandamizi wa Ulinzi wa Amani kutoka SADC, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na Taasisi za Serikali za kiraia kutoka Tanzania.
Meja Jenerali Mzee amesema ni muhimu nchi wanachama wa SADC kujitahidi kushiriki katika mafunzo mbalimbali yanayotolewa kuhusiana na ulinzi wa amani ili kupata uelewa wa pamoja ambao utakuwa nguzo muhimu katika utekelezaji wa majukumu yao hasa ya ulinzi wa amani.
“Wanapofanya mafunzo hayo kwa pamoja wanapata uelewa mmoja wa kutekeleza majukumu yao, wasipofanya hivyo wanaweza kutofanikiwa. Nisisitize wale wanaoshiriki kwenye jukumu la ulinzi wa amani wakipata mafunzo haya yatawasaidia kufanya majukumu yao kwa weledi na ufanisi mkubwa,” amesema Meja Jenerali Mzee na kuongeza
“Kumekuwa kukijitokeza changamoto katika nchi zetu na duniani kwa ujumla ambazo zinasababisha watu kuuawa na kushambuliana, hivyo chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa (UN) zipo juhudi za kulinda amani ambazo zimegawanywa katika kanda, Kwa Afrika ukanda ni SADC, mafunzo haya yamewakusanya wajumbe kutoka nchi hizo ambapo wanakutana na kupewa kozi hiyo muhimu katika utekeleza wa jukumu la ulinzi wa amani,” amesema
Naye Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania, Brigedia Jenerali George Itang’are amesema kozi hiyo ni kubwa kuliko zote zilizoendeshwa kwa walinzi wa amani na kwa mara ya kwanza inatolewa Tanzania na kwamba ni kozi ya pili Kikanda.
“Sisi kama chuo tunaendesha kozi mbalimbali ila hii ya leo ni ya kwanza kufanyika hapa nchini na lengo kubwa ni kutoa fursa kwa maofisa wakuu ambayo wataenda kwenye ulinzi wa amani katika nchi mbalimbali chini ya UN na SADC kupata uelewa wa pamoja,” amesema Brigedia Jenerali Itang’are
Written by Janeth Jovin