Bongo5 Makala

Makala: Kolabo 8 za kimataifa zinazosubiriwa Bongo (+Audio)

Wasanii wa Bongo Flava wamekuwa wakipambana kuhakikisha wanaupeleka muziki huo nje ya nchi na duniani kwa ujumla.

Kufanya kazi na wasanii wa nchi nyingine ni njia moja wapo wanayoitumia wasanii hao ili kufikisha muziki huo katika nchi hizo. Pia wasanii hutumia njia hii kama sehemu ya wao kujitangaza zaidi.

Hapa tumekuletea kolabo ambazo wasanii wa Bongo waliweka wazi kuzifanya na wasanii kutoka nchi mbali mbali lakini hadi sasa hazijatoka ingawa zinatajibiriwa kuja kufanya vizuri kutokana na uzito wa wasanii hao.

1. Alikiba X Yvonne Chaka Chaka

December 15, 2016 ilikuwa ni siku ya furaha kwa mashabiki wa Alikiba mara baada ya muimbaji huyo mwenye sauti ya aina yake kuweka wazi kuwa amefanya ngoma na msanii mkubwa na mkongwe Afrika, Yvonne Chaka Chaka.

Ilikuwa si stori ya kuchukulia poa kwa msanii wa Tanzania kufanya kazi na Yvonne Chaka Chaka a.k.a Princess of Africa ambaye amekonga nyoyo za mashabiki wake kwa kipindi cha miaka 29 sasa. Mashabiki wake wamechiziki vilivyo na ngoma kama I’m Burning Up, Thank You Mister DJ, I Cry for Freedom, Makoti, Motherland na nyinginezo kibao.

Siku hiyo Alikiba aliandika katika ukurasa wake wa Instagram; ‘It was a great honor and pleasure to meet Mama Yvonne Chaka Chaka who I have loved and admired all my life . Thank you for hosting us and sharing your memories, advices and guidance. I am truly grateful and looking forward to our project,”.

Kuanza hapo mashabiki wake wakawa wanangojea ngoma hiyo. July 6, 2017 katika mahojiano na XXL ya Clouds FM, Alikiba alisema wimbo huo upo tayari lakini kuna ratiba lazima ziwepo sio tu wimbo umefanyika tu na kuotoa ila aliwahakikishia mashabiki wake kila wimbo utatoka kwa muda wake.

2. Harmonize X Tyga

March mwaka huu boss wa label ya WCB, Diamond Platnumz ndio aliweka wazi kuwa kuna kolabo inakuja kati ya Harmonize na Tyga kutokea nchini Marekani.

“Kuna nyimbo kafanya na wasanii wa ndani na nje. Harmonize ana nyimbo mpaka na Tyga, ana nyimbo Harmonize na Tyga amefanya,” alisema Diamond.

Licha ya Harmonize kufanya kolabo na Tyga, wasanii hao wajawahi kuonana uso kwa uso, bali ni makubaliano ya menejiment za pande zote mbili kisha wasanii hao wakafanya wimbo kwa mtindo wa kutumiana sauti. Hilo alilieleza Harmonie wakati wa mahojiano na Radio Five.

Kukamilika kwa kolabo hiyo na kutoka kutamfanya Harmonize kuwa msanii wa tatu kutoka WCB kufanya kazi na wasanii wakali kutoka Marekani mara baada ya Diamond aliyefanya na Ne-Yo na Rick Ross, huku Rayvanny akifanya na Jason Derulo.

3. Vanessa Mdee X Major Lazer

Si kufanya wimbo tu, Vanessa Mdee na kundi la watayarishaji wa muziki kutokea Marekani, Major Lazer tayari walionekana location kwa ajili ya ku-shoot video ya ngoma yao.

April 17, 2017 mara baada ya Vanessa kutoka ku-perform kwenye tamasha la Gidi nchini Nigeria, ali-share picha katika ukurasa wake wa Instagram zikionyesha wakiwa location na Major Lazer.

Hii ilikuwa ni stori moja ya kibabe sana katika Industry ya burudni Bongo, kivipi?. Kundi la Major Lazer linaongozwa na Diplo ambaye ameweza kutayarisha ngoma mbili katika albamu ya Beyonce, Lemonade. Tuachane na hilo.

Katikati ya November 2017 Vanessa Mdee alifunguka kwanini hadi sasa kolabo na Major Lazer haijatoka kwa kueleza kuwa kolabo hiyo ni ya kundi hilo (Major Lazer), hivyo wao ndio wenye mamlaka ya kuamua lini itoke.

4. Alikiba X Davido

Hapo awali kulikuwa na tetesi kuwa Alikiba na Davido wana ngoma waliyofanya pamoja ila hakuna aliweza kuthibitisha hilo.

Tatimaye July 2015 katika Red Carpet ya tuzo za MTV MAMA, Davido akaamua kumwaga mchele kwenye kuku wengi kwa kueleza kuwa kolabo na Alikiba ipo na siku si nyingi itatoka.

“I have a song coming out with Alikiba too, that’s gonna be crazy,” alisema Davido.

Hata hivyo July 2017 Alikiba alikuja kukanusha taarifa hizo kwa kueleza hakuna ngoma iliyofanyika ila kuna mipango ya kufanya endapo muda utapatikana.

“Unajua wasanii muda mwingine tunakuwa na maneno ya kuridhisha watu lakini kiukweli hakijafanyika chochote ila plan zipo za kufanya na muda tukiupata tutafanya ila sijajua ni lini,” alisema Alikiba.

Kwa maelezo ya Davido na Alikiba kuna uwekano wa kutokea chochote kati yao, endapo ikiwa ndivyo basi tuhesaba hiyo ni hit song ya aina yake.

5. Weusi X Sauti Sol

August 2015 kundi la Sauti Sol kutokea nchini Kenya lilikuwepo Tanzania kwa ajili ya media tour, katika mahojiano na FNL ya EATV waliweka wazi baadhi ya kolabo walizofanya na wasanii kutoka kwenye Bongo Flava.

Wasanii waliotajwa ni pamoja na Alikiba, Ommy Dimpoz, Weusi, Fid Q na Vanessa Mdee, pia waligusia kolabo yao na Yemi Alade kutokea nchini Nigeria.

Mwaka uliofuata, September 2016, rapper Joh Makini alithibitisha kukamilika kwa kolabo hiyo na kinachosubiriwa ni vitu vichache ili waweze kuitoa.

Hii nayo ni moja kolabo ambazo zinasubiriwa kwa hamu kutokana inakutanisaha makundi mawili ya muziki. Kutoka kwa ngoma yao kutalifanya kundi la Sauti Sol kuwa na kolabo mbili nchini Tanzani baada ya ile waliyofanya na Alikiba na AY.

6. Izzo Bizness & Abela (The Amaizing) X Ycee

Mwishoni mwa August, 2017 Ycee kutokea nchini Nigeria alikuja kufanya media tour Tanzania, ndipo alipokutana na Izzo Bizness na Abela Music wanaounda kundi la The Amazing.

Kukutana kwao haikuwa bure bali waliingia studio na kurekodi ngoma ambao ulisimamiwa na producer Abba.

February, 2018 katika mahojiano na Bongo5 Izzo Bizness alisema kinachokwamisha kolabo hiyo kutoka ni ku-shoot video pekee ila wameshawasiliana na meneja wa msanii huyo na kuna hatua fulani wamefikia.

7. Rosa Ree X Emtee

Rosa Ree ambaye kwa sasa anafanya vizuri na ngoma ‘Marathon’ aliyomshirikisha Bill Nass, March 23, 2018 aliingia studio na Emtee kutokea nchini Afrika kusini.

Kwa takwimu za mwaka 2015 Emtee ni miongoni mwa marapa watatu wanaochezwa zaidi nchini humo. Hivi karibu Rosa Ree aliweka wazi kuwa video ya wimbo waliourekodi ipo tayari.

Kukamilika kwa ngoma hii na kutoka kutamfanya Rosa Ree kuwa na ngoma tatu ambazo ameshirikisha marapa wenzake baada ya kufanya hivyo kwa Khaligraph Jones na Bill Nass.

8. Rostam X Khaligraph Jones

Kundi la Rostam ambalo linaundwa na Roma na Stamina September 2017 walikuwa na media tour nchini Kenya ndipo walipokutana na Khaligraph Jones.

Kukutana kwa hawa marapa watatu haikuwa bure bali waliingia studio na kurekodi ngoma. April 2018 Rostam walirudi tena nchini kwa ajili ya ku-shoot video ya ngoma hiyo.

Khaligraph Jones ambaye ameshafanya kolabo na wasanii wa Bongo kama Young Killer, Rayvanny, Christian Bella, Chin Bees, Nikki Mbishi na Rosa Ree, anatajwa na mtandao wa Africa Ranking kama rapper tisho zaidi akifunga top 10 ya wale wakali kutoka Afrika.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents