Bongo5 Makala

Makala: Kuna muziki na mapenzi, pia kuna muziki, mapenzi na kiki (+Audio)

Kwa tabasamu lilojaa kila aina ya utani kutoka kwa mchekeshaji Mpoki atakueleza kuwa mapenzi yana nguvu kuzidi breakdown, huku nguli wa muziki Marehemu Remmy Ongala akiimba wimbo, Mziki Asili Yake Wapi.

Achana na hao: Mapenzi ni hisia kali za upendo ambazo humfanya mtu kujisikia furaha na amani katika moyo wake. Kumbuka kuna mapenzi yenye dhamira ya kuridhishana kingono na yale ya urafiki wa kawaida.

Kamusi ya kiswahili inaeleza kuwa muziki ni aina ya sanaa yenye mpangilio wa ala na uimbaji unaoleta athari fulani kwa kiumbe. Baadhi ya sifa za muziki ni uzito wa sauti (pitch) na mahadhi (rhythm).

Muziki na Mapenzi

Siwezi kukupa maana ya muziki na mapenzi ila ni vitu viwili ambavyo vinaenda pamoja na vimebeba nguvu kubwa ndani yake. Kila kimoja kina nguvu isiyoweza kuelezeka kwa lugha ya kawaida au rasmi na kueleweka.

Mwanamuziki nguli wa miondoko ya Rock na Blues, Elton John alipata kusema; Muziki una nguvu ya uponyaji amini usiamini, ndio tiba pekee duniani inayoweza kukutoa kutoka kwenye lindi la mawazo na maumivu angalau kwa saa chache.

Nguvu ya muziki anayoibanisha hapa Elton John ni ipi?. Utafiti wa Loma Linda University nchini Marekani katika kitengo chao cha afya unaeleza kuwa wagonjwa 100 waliowekwa katika chumba chenye muziki bila kupewa dawa walipona haraka kuliko waliopewa dawa, hiyo ndio nguvu ya muziki.

Je kuna nguvu ya mapenzi?. Baada ya kutoka gerezani hivi karibuni Mbuge wa Mbeya Mjini ambaye pia ni msanii wa hip hop Bongo, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ aliweka picha katika ukurasa wake Instagram ikimuonesha akiwa na mkewe na kuandika;

Bonnie and Clyde, if you know what I mean. Amesimamia vema ‘SHOW’ wakati Mbunge yuko jela, she did a great job standing by her nigga.

Hapa topic sio Sugu, ni watu wawili aliowataja mwanzoni mwa sentensi yake, yaani Bonnie and Clyde. Bonnie ni mwanamke na Clyde ni mwanaume.

Mwaka 1996 msanii wa muziki wa hip hop nchini Marekani, Tupac alirekodi wimbo uitwao Me and My Girlfriend ambao unapataika katika albamu yake ya tano, The Don Killuminati: The 7 Day Theory iliyotoka November 05, 1996.

Katika wimbo wa Me and My Girlfriend, Tupac ndipo anawagusia Bonnie na Clyde kwa kueleza jinsi mapenzi na girlfriend wake yanavyoenda kama ya wawili hao ambao walizaliwa mwanzoni mwa karne ya 19, Bonnie alizaliwa October 01, 1910 wakati Clyde alizaliwa March 24, 1909.

Bonnie na Clyde

Bonnie na Clyde ni wapenzi waliopendana sana kwa dhati hata hivyo maisha yao upande wa pili yalikuwa yenye histori mbaya kwa kuwa yalijaa uhalifu, umafia, visasi, mauaji nakadhalika.

Walipendana sana na waliogopa kusalitiana kutokana hakuna kati yao aliyeogopa kupoteza maisha ya mwenzake. Kutokana na uhalifu wao wakipoteza maisha siku moja wote wawili, hiyo ilikuwa May 23, 1934.

Hivyo ndivyo tunaweza kueleza maana ya muziki na mapenzi, muingiliano wa vitu hivyo viwili na nguvu iliyopo katikati.

Kwanini Muziki, Mapenzi na Kiki

Mwanamuziki wa zamani, Remmy Ongala aliyefariki December 12, 2010 katika wimbo wake ‘Mziki Asili Yake Wapi’ alitoa maana kadhaa za muziki.

“Muziki asili yake wapi? muziki ni wa nani? muziki hauna mwenyewe, muziki ni maombolezo,” ndivyo anavyoanza katika wimbo huo. Remmy alisema muziki ni; wimbo, fundisho, maombolezo kilo.

Katika maana hizo na pamoja na nguvu ya muziki hakuna sehemu ambayo unaona uhusiano wa vitu hivyo na kiki kama ambavyo kwa sasa unaonaka katika Bongo Flava. Najua bado hujanielewa.

Kilichonisukuma kuandika Makala haya ni baada ya kuona hivi karibuni mtindo wa kutumia ‘kiki za kimapenzi’ kama sehemu ya kutangaza muziki. Ni wasanii wachache sana ambao hawazingatii hilo katika muziki wao.

Twende kwa Mifano

Wiki iliyopita kulikuwa na mvutano mkubwa kati ya mchekeshaji MC Pilipili na Muigizaji Mwijaku, chanzo cha ugomvi wao ilielezwa kuwa ni Mwijaku alimuoa Nicole ambaye aliwahi kuwa mpenzi wa MC Pilipili.

Mvutano wao ulioneka kuwa mkubwa kwa kutupiana maneno ya hapa na pale. Wote kwa pamoja walifanya mahojiano na baadhi ya vyombo vya habari huku kila mmoja akimuongelea ndivyo sivyo mwenzake.

Mwisho wa siku ikaonekano wote wameshiriki katika video ya wimbo mpya wa Mrisho Mpoto na Harmonize uitwao Nimwage Radhi. Bila shaka hawa walitumika kama sehemu ya promotion ya wimbo huo.

Kitu hicho ni kama walichokifanya Lulu Diva na Rich Mavoko kabla ya kutoa wimbo wao mpya unaokwenda kwa jina la Ona. Licha ya mara kadhaa kukanusha kuwa wao si wapenzi lakini pindi walipokaribia kutoa wimbo wao walitaka kufanya suala hilo ni rasmi na kutaka watu waamini kuwa ndivyo lilivyo kwa sasa.

Pia Rayvanny alifanya hivyo wakati yupo mbioni kutoa wimbo ‘Safari’, kabla ya kutoa wimbo kulikuwa na taarifa za yeye kuachana na mzazi mwenzie, Fahyma taarifa ambazo yeye ndiye aliyezianzisha, mwisho wa siku Fahyma akaonekana katika video ya wimbo huo.

Kama visa vya kimapenzi kinaunza zaidi muziki wa wasanii kwa sasa, basi waelewe kuwa kuna visa vingi vya kimapenzi ambavyo vingeuza zaidi kuliko vile ambavyo wanavitengeneza wao.

Mwaka 2003 Jay Z kwa kushirikiana na mkewe, Beyonce waliuridia wimbo wa Tupac ‘Me and My Girlfriend’ uliotoka mwaka 1996. Sababu kuu ya kufanya hivyo ni kutokana na kisa cha kimampezi cha Bonnie na Clyde kama nilivyotangulia kueleza.

Inawekana watu aina ya Bonnie na Clyde wasiwepo Bongo kabisa lakini kuna matukio mengi ya kimapenzi yenye kubeba ujumbe mpana katika wimbo kuliko visa vya kutengeneza.

Mfano ni kifo cha Rapper Saimon Sayi a.k.a Complex na mpenzi wake Vivian Tillya kilichotokea August 21, 2005. Walifariki wakiwa njiani wakati Vivian anaenda kumtambulisha Complex nyumbani kwao kama mpenzi wake.

Tupac aliimba kisa cha Bonnie na Clyde baada ya miaka 62 tangu walipofariki wawili hao, Jay Z na Beyonce walifanya hivyo baada ya miaka 69, je ina maana wasanii wetu hawasomi historia na ndio sababu ya kutengeza matukio yao binafsi?.

Hathari Zake

Suala ni kwamba wapo wanaoamini kuwa visa vya kutengeneza vinasadifu maisha ya uhalisi ya wanamuziki wengi kitu ambacho si kweli. Msanii ni mtu ambaye anaweza kujivika uhusika ambao utamtenga mbali kabisa na maisha yake kawaida.

March mwaka huu Mtangazaji wa kipindi cha Ladha 3600 cha E FM, Jabir Saleh aliiambia Bongo5 kuwa watu wa media waache ku-support vitu visivyo vya msingi kwani kuna vipaji vingi vipya vinatakiwa kuinuliwa ila vinakosa hiyo nafasi.

Alienda mbali zaidi kwa kueleza kuwa miaka ya hivi karibuni wasanii wa Bongo wamekuwa wakikimbizwa na wale mataifa ya Afrika Magharibi hasa Nigeria katika tuzo kubwa Afrika kutokana na kuendekeza kitu alichoita ‘kiki’.

Hivi karibuni kituo cha runinga cha BET kilitangaza majina ya wasanii watakaowania Tuzo za BET 2018 kutoka Afrika katika kipengele cha Best International Act, hata hivyo hakukuwa na msanii yeyote kutoka Tanzania, hii ni baada ya Diamond kuwania kwa mwaka 2014 na 2016

Hivyo ni vema muziki ungebaki wenyewe ili uweze kujitangaza wenyewe bila kuutengenezea visa au matukio ili ujitangaze. Kuendelea kufanya hivyo ni kunufaisha zaidi vyombo vya habari ambavyo hutegemea visa au matukio hayo kama sehemu ya kufanya biashara ila hakuna faida ya moja kwa moja kwenye muziki wa msanii husika.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents