Bongo5 Makala

Makala: Kwa inavyoonekana bora kuitwa Underground kuliko Mkongwe

Kadiri siku zinavyozidi kusonga ndiyo na muziki wa Bongo Flava unabadilika. Mabadilio yanaambatana na changamoto zake, maswali yenye kuhitaji majibu ya kufikirisha zaidi n.k.

Kwa sasa kuna mjadala katika Bongo Flava, kupata tafsiri ya yupi hasa ni msanii Mkongwe. Huku wengine wakitabainisha kuwa kuitwa Mkongwe ni njia ya kuondolewa katika mfumo wa kiashara kwa upande wa muziki huo.

Kwa mujibu wa kamusi ya kiswahili ya Oxford inaeleza kuwa Mkongwe ni mtu mwenye umri mkubwa sana, mzee sana na asiyejiweza.

Hivi karibuni rapper Nikki Mbishi kupitia mtandao wa twitter aliandika; Wasanii wakongwe wa Tanzania wengi wao hawana miaka 40 ya kuzaliwa ila wanazeeshwa ili wajione hawawezi kasi ya watoto wa ’98 au 2000′, sasa kama Dully Sykes mkongwe R. Kelly je?’.

Kauli hiyo ya Nikki ilikuja baada ya msanii Q Chief kutangaza kuacha muziki kutokana na mambo ambayo aliona hatendewi haki katika tasnia ya muziki au hayapo sawa kwa upande wake.

May 23, 2018 katika mahojiano na XXL ya Clouds FM, Q Chief alisitisha mpango wake wa kuacha muziki, hivyo ataendelea kutoa ngoma kama kawaida. Hilo bado linangojewa.

Siku kadhaa mbele rapper Wakazi alieleza kuwa hamna kitu kinaboa kama Wasanii wakongwe ambao kila kukicha wanaenda kulia kwenye media ili wapewe msaada wa kuendeleza muziki wao.

“Kama nyie mkilia, je wasanii wachanga (who look up to you) na hawajawahi kutoka wafanyaje?! Why don’t you be grateful for a glorious past & cherish it,” alihoji Wakazi kupitia mtandao wa Instagram.

Hata hivyo kwa upande wa TID alieleza kuwa wasanii wanapewa jina la Ukongwe ili kukoseshwa baadhi ya fursa muhimu ambazo wana haki kuzikipata na ndicho kilichotokea kwa Q Chief.

Katika mahojiano na Refresh ya Wasafi TV alisema kitu hicho kilimtokea yeye baada ya kuanza kudai maslai yake, hivyo akawekwa pembeni na kuambiwa muda wako umepita.

“Legends ni mwanamuziki ambaye ana miaka zaidi ya 50 kwenye game, mimi unaniita Legends gani?, nimeanza muziki miaka 19 nyuma hata miaka 40 sijafikisha, sisi ndio tunatakiwa tule matunda.

“Ni kukutoa kwenye line ili kuwaweka watu wao, kwa vile sisi tunawadai wametuzulumu sana. So Diamond was me lakini wakasema wewe siunajifanya mjanja sasa tunamleta Diamond tukushushe wewe,” alisema TID.

Hata hivyo msanii Roma katika mahojiano na FNL ya EATV alieleza kuwa wasanii wana haki ya kukataa kuitwa Wakongwe. Pia aliongeza kuwa tatizo halipo kwenye jina hilo bali kuna baadhi ya makundi hayapewi nafasi kwenye media.

“Snoop Dog ni mzee anafanya mchongo na Wiz Khalifa, kwanini Mox asifanye mchongo na Country Boy halafu ukawa kweli mchongo lakini sisi tunakuja kuitafsiri Mkongwe hana nafasi kwenye generation ya sasa hivi which is total wrong,” alisema Roma.

Roma aliongeza kuwa ikiwa msanii ataitwa Mkongwe lakini anapata kile ambacho anastahili wala hakuna ambaye angelaumu au kukataa jina hilo.

Kwa upande wake Dully Sykes anakiri kuwa yeye ni Mkongwe katika Bongo Flava na haoni noma kuitwa jina hilo kwani amepambana na muziki wa Bongo tangu mwaka 1999.

“Kuna vitu vingi nimevifanya, kwa hiyo mimi ni Mkongwe kwa miaka yote niliyofikia, kwa ukongwe ni heshima. Siwezi kukataa mimi sio Mkongwe, kwa yeyote atakayekataa yeye amekataa lakini mimi ni Mkongwe,” Dully aliiambia Refresh ya Wasafi TV.

Hata hivyo kwa upande wake Lady Jaydee ambaye ni msanii pekee wa kike Bongo mwenye albamu nyingi zaidi, anaona si sawa kuitwa msanii Mkongwe kwa sasa.

“Mnikome, Mkongwe Bichuka na Khadija Kopa?, tena mniache kabisa mimi bado mbichi,” aliandika Lady Jaydee katika mtandao wa Twitter.

Hivyo kwa mtanzamo wa wasanii karibia wote hapo juu utaona ni bora msanii yeyote wa Bongo Flava ambaye ananyemelewa na jina hilo ni bora akaitwa jina lingine hata chipukizi (underground) ikibidi kuliko Mkongwe.

Je, Mkongwe ni nani?

Kama nilivyotangulia kueleza kuwa Mkongwe ni mtu mwenye umri mkubwa sana, mzee sana na asiyejiweza. Je, wasanii wa Bongo Flava wanaoitwa hivyo wamefikia hatua hiyo?, hapana!.

Je, Ukongwe unaozungumziwa katika Bongo Flava unatokana na umri, mchango wa msanii husika katika tasnia, heshima yake au ni kuandaliwa mazingira ya kuondolewa kwenye muziki huo na kupisha wengine?. Tujadili kwa pamoja. Nawasilisha.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents