Bongo5 MakalaDiamond PlatnumzLady Jay DeeWema Sepetu

Makala: Muda si rafiki kwa Chid Benz kumpatia anachotaka (+video)

Katika wimbo wa Fid Q August 13 aliyomshirikisha Juma Nature, katika verse ya pili ya ngoma hiyo kuna mistari Fid anasema, “Chagua ufe kijerumani uanguke na tai shingoni, au mchaga anayeshinda njaa wakati anazo hela mfukoni, huu si muda wa kujaribu wenzako wanafanya kweli au hujui bahari tulivu haimpimi nahodha wa meli”.

Kwa tafsiri isiyo rasmi Rapper huyo mkongwe kutoka Rock City, Mwanza anataka tuelewe kuwa ni vema kuamua kupigania kile unachotaka ili kujitengenezea heshima yako na kutoridhika mapema, pia hakuna muda wa kupoteza ingawa changamoto ni nyingi katika mapambano hayo. Weka nukta hapo.

Karibu Chid Benz

Kwa sasa anaonyesha dalili ya kupigania kile ambacho anakita katika muziki wake baada ya kutumbukia katika wimbi la matumizi ya dawa za kulevya kwa kipindi kirefu, amekuwa akijaribu kurudi lakini kwa bahati mbaya hujikuta amerudi tena katika janga hilo.

June 22 mwaka huu Chid Benz aliteka upya spika za redio zetu kwa kudondosha ngoma mpya ‘Muda’ aliyomshrikisha Q Chillah, kabla ya hapo tayari Q Chillah alikuwa amethibitisha kuwa kuna kazi ya pamoja inakuja. Kauli ya muimbaji huyo mwenye historia ya pekee zaidi katika Bongo Flava ilizidi kuwapa mashabiki kiu ya kuhitaji ngoma hiyo.

Kiu inatokana na historia ya maisha ya Q Chillah ambayo amewahi kupitia huko nyuma ambayo haitofautiana na mwenzake. Chillah ameshawahi kuwa mwathirika wa dawa za kulevya lakini kwa mapenzi yake binafsi aliamua kuonndoka huko kitu ambacho amekuwa akisisitiza hata Chid Benz anaweza kufanya hivyo iwapo tu yeye binafsi ataamua kutoka moyoni.

Sasa mashabiki wanaposikia hawa wawili kwa pamoja wana ujumbe ambao wanataka kuutoa ni lazima kiu ipande kwa ghafla, na kweli ngoma waliyoitoa imeshusha kiu ya wengi kama si kuimaliza kabisa.

Lakini ikumbukwe huu si ujio wa kwanza kwa Chid Benz tangu alipoingia matatizoni, amekuwa akija na kutoa ngoma kisha anapotea. Nakumbuka mwaka jana alikuja kwa kishindo akiwa support ya WCB na kutoa wimbo pamoja na Rayvanny uitwao Chuma, baada ya hapo ulifatia ukimya bila hata video ya ngoma hiyo, pia kuna kolabo alishafanya na Diamond & AY ‘Mpaka Kuche’ nayo ikawa hivyo hivyo.

Kwani Chid Benz anataka nini?

Chid anataka kurudisha heshima yake kubwa aliyokuwa nayo katika Bongo Flava lakini hataki kufa kijerumani. Bila kupindisha maneno Chid ni msanii aliyefanya kazi na wasanii karibia wote wakubwa katika Bongo Flava, ngoja nikukumbushe kitu.

Sauti yake imeshakaa katika ngoma moja na wasanii kama Diamond, Alikiba, Lady Jaydee,  Mwasiti, K Lyinn, Marlaw, Tunda Man, Spack, Ben Paul na TID wakiwa ni miongoni mwa wale wanaofanya muziki wa kuimba.

Pia alijenga ufalme wake katika rap/hip hop kwa kufanya kazi na wasanii kama Fid Q, Na 2 Nako Soldiers, Marehemu Geez Mabovu, JCB, Jay Moe, Stamina, Nikki Mbishi, One the Incredible, Songa, Izzo Biziness, Stereo, Prof Jay, Marehemu Mangwea,  Mwana FA, Lord Eyes, Babuu wa Kitaa, Mansu-Lii, Baba Johnii, County Boy, Climax Bibo, Young Dee, Marehemu Langa na Mh Temba.

Kama hiyo haitoshi pia aliwahi kushirikiana na wakali wa muziki taaribu kama Mzee Yuseph ambaye kwa sasa ameacha muziki huo na Khadija Kopa. Picha inayonijia nikitazama orodha hii ni kwamba kipindi cha nyuma Chid Benz alikuwa akihitajika zaidi katia kolabo na hata yeye alipohitaji muhusika aliona hiyo ni kama fursa kwake.

Lakini muda huo ulishaondoka na haupo nae tena, anaweza kujivunia kazi kubwa aliyoifanya na pia ndani yake kuna lawama kama sio majuto kwa nini hanufaiki na kazi hiyo, pengine muda ungemgoja hadi saa bila shaka angekuwa ni miongoni mwa msanii wanaojimuda zaidi kiuchumi lakini tatizo muda umemkatili.

Kwa nini Muda

Muda kwa sasa si rafiki wa kumpatia Chid Benz kile ambacho anaamini anastahili kupata, uzuri ni kwamba yeye mwenyewe analijua hilo ila hana jinsi zaidi ya kuweka machungu yake katika ngoma anazokuwa anatoa katika nyakati hizi.

Ukisikiliza kwa makini ngoma mpya ‘Muda’, chorus aliyofanya Q Chillah inaweka wazi hilo, ni asiye na akili timamu pekee ndiye anaweza kupinga ukweli huo.

https://youtu.be/ZM3v0qzXmzs

“Muda niliopoteza hawawezi kufidia, ghrama na maumivu hawawezi kufidia, Dar es Salaam bila king kong is not true, Dar es Salaam bila chuma we back mikono juu”. Anakumbuka muda alioupoteza katika matumizi ya dawa za kulevya, maumivu na gharama ni vitu ambavyo hakuna anayeweza kufidia.

Je ni nani anaweza kumlipa fidia Chid zaidi ya mziki wake?, bila shaka hakuna na ndio sababu ya kupigania nafasi yake, pia anaeleza alipokuwa nje ya muziki watu wake kuna vitu walivikosa ila sasa amerudi.

Hata hivyo kwa nafasi ilivyo kwa sasa kwenye game hata yeye pamoja na muziki wake ni vigumu kulipa fidia anayodai kwani mambo yamebadilika tena sana. Waimbaji  na wachanaji ni wengi ukilinganisha na kipindi alichokuwa akifanya vizuri, na kanuni ya biashara ni kwamba uzalishaji ukiwa mkubwa/juu na bidhaa hushuka bei, hivyo kuitajika kwa Chid si kama mwanzo.

Kwa maana hiyo muda huu si wa Chid Benz tena, hivyo uwezekano wa kupta anachotoka ni mdogo na kwa kulitambua hilo anakaandika ngoma ya Muda ili watu waelewe maumivu yake.

Ushauri wangu kwa Chid Benz

Wakati anatambulisha ngoma yake alitupa lawama nyingi kwa Babu Tale kuwa alishindwa kumvumilia wakati walikuwa na mipango ya kufanya vitu vingi na kufika mbali. Hili ni kosa ambalo Chid litaendelea kumgharimu na hata wasanii wenye tabia hii, kuamini sitaweza kufika sehemu fulani bila mtu fulani au ningekua pale kama si fulani alinikwamisha.

Kama nilivyotangaulia kueleza hapo awali ni lazima Chid aamue kufa kijerumani kutetea heshima yake, kipindi ambacho amekuwa nje ya game kuna mambo mengi yamebadilika ni lazima akubali kuendana na mazingira ya sasa.

Kama Fid Q alivyoeleza ‘huu si muda wa kujaribu wenzako wanafanya kweli’. Ni mwezi sasa umepita tangu aachie ngoma yake ‘Muda’, sijaona promotion yoyote aliyofanya, media tour si kwa kiwango kile, na video ya ngoma yenyewe haijatoka. Kwa mtindo huu ni vigumu kulishika soko ambalo ndani ya mwezi mmoja msanii anatoa ngoma tatu zenye viwango vya kimataifa pamoja na video zake na promotion ya hatari.

Ingawa tunafahamu kuwa Chid ni mchaga anayeshinda njaa wakati hela anazo mfukoni, yaani ni msanii mkubwa mwenye mashabiki wake anatakiwa kuelewa kuwa kuna kazi kubwa anapaswa kufanya kwa sasa kutoa ngoma pekee haitoshi.

Ni kweli hakuna anayeweza kulipa muda wako, gharama na maumivu ila hiyo isikupe sababu ya kufanya katika kiwango cha kawaida, mitihani na misukosuko unayopitia kwa sasa ndicho kipimo cha dhamira yako ya kutaka kurejea kwani bahari tulivu haimpimi nahodha wa meli.

By Peter Akaro

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents