Bongo5 Makala

Makala: Tumpime Godzilla kwa mizani ya Alikiba na Diamond (+Audio)

Ukitaja orodha ya marapa 10 Bongo wa miaka ya hivi karibuni, utafanya makosa bila kulihusisha jina la Godzilla. Mwenyewe anapenda kujiita King Zilla akiwakilisha vyema eneo analotokea, yaani Salasala.

Hivyo hivyo unapotaja wasanii wanaoimba wenye mashabiki wengi na wanaokodolewa macho na wengi kwa sasa, ni vigumu kutowataja Alikiba na Diamond. Kwa sasa hawa ndio wanatajwa kama wasanii wenye ushindani mkubwa kimuziki Bongo.

Kwanini Godzilla

Rapper huyo ambaye inadaiwa nafasi yake kwenye game imechukuliwa na Bill Nass ingawa hakuna uthibitisho sahihi wa hilo, aliweza kushirikiana na waimbaji wote wawili. Wakati huo bado kazi zake nyingi zilikuwa zikifanyika MJ Records.

Producer kutoka MJ Records, Zachaa ndiye aliyesimamia kolabo kati ya Godzilla na Diamond ambapo walitoa wimbo uitwao Mtoto wa Mama. Weka nukta hapo.

Godzilla alikuja kumshirikisha Alikiba katika wimbo wake uitwao Milele. Ni wimbo ambao ulimuweka rapper huyo sehemu nyingine tofauti kabisa kimuziki ukilinganisha na mwanzoni ilivyokuwa.

Ni mara chache kumsikia Alikiba kwenye kolabo za namna hiyo, ilimchukua muda kidogo hadi pale Mwana FA alipokuja kumshirikisha muimbaji huyo katika wimbo wake unaokwenda kwa jina la Kiboko Yangu. Pia ilichukua muda zaidi hadi pale alipokuja kusikika katika ngoma ya Mr. Blue iitwayo Mboga Saba.

Kwa haraka haraka tunaweza kusema kuwa Gozdilla, Mwana FA, na Mr. Blue ni miongoni mwa wachanaji wachache Bongo waliofaidi sauti ya Alikiba katika chorus za ngoma zao.

Ngoma ya Mwana FA ‘Kibo Yangu’ inaonekana kuwa na mafanikio zaidi kati ya hizo tatu nilizozitaja. Mwaka 2015 iliweza kushinda tuzo ya Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA) kama wimbo bora wa kushirikiana. Baada ya hapo tunaweza kuitazama Mboga Saba ya Mr. Blue kwa idadi ya views katika mtandao wa YouTube ambapo hadi sasa ina views zaidi ya Milioni 2.

Mwisho kabisa ni hiyo ya Godzilla ‘Milele’, licha ya kufanya vizuri mtaani bado ni vigumu kupima mafanikio yake kutokana haikushinda tuzo yoyote wala haina official video. Kupima mafanikio yake kwa kuangali chart za radio station ni kujidanganya kwa kuwa kuna baaadhi zinaendeshwa kishikaji tu.

Mifano Zaidi

Kuna baadhi ya wasanii ambao kufanya kwao kolabo kati ya Alikiba au Diamond kuliweza kuwafanya kuiteka mitaa kitu kilichowapa show zaidi. Hii ni kutokana na kuunganisha mashabiki wa pande zote mbili na si kana kwamba kulizaliwa wengine wapya.

Nay wa Mitego na Shetta ukiwauliza uzito wa kolabo walizofanya na Diamond katika maisha yao ya kimuziki wanaweza kupata tabu kukupa takwimu za kimafanikio ila kweli walifanikiwa zaidi.

Producer Mr. T Touch aliwahi kueleza kuwa Nay wa Mitego hajawahi kutoa hit nyingine zadi ya Muziki Gani ambayo alimshirikisha Diamond. Ngoma hii ilimfanya kupiga tour kubwa Tanzania kupitia tamasha la Fiesta, hivyo hivyo kwa Shetta alipomshirikisha Diamond katika wimbo wake uitwao Nidanganye.

Je, ni kweli kuna faida walipata?, ndiyo, pasina shaka kuna kitu kizuri walikipata na ndio sababu ya wote wawili kuja kufanya kolabo nyingine na Diamond. Tuachane nao.

Hivi karibuni Nuh Mziwanda akihojiwa na Wasafi TV alieleza kuwa kolabo na Alikiba ilimfanya kupiga tour Tanzania nzima. Tour ilichukua zaidi ya miezi mitatu na kumuwezesha kujikusanyia fedha hadi aliposimamisha mjengo wake.

Pia ndio wimbo pekee wa Nuh Mzinda kufikisha viewes zaidi ya Milioni 2 katika mtandao wa YouTube tangu alipoanza muziki.

Kwa hayo machache utaona ni kwa namna gani kolabo na hawa waimbaji wawili wanaotajwa kuwa na ushindani zaidi Bongo zilivyo na manufaa. Je, ndivyo ilivyokuwa kwa Godzilla?.

Ni mapema kusema hapana na ni vigumu kusema kuna mafanikio ila ndani yake kuna somo pana. Hapa kuna jambo, hakukuwa na mkakati wa kibiashara kabla ya kutoa ngoma husika, kama alitoa kwa ajili ya mashabiki wake kufurahi tu, ni sawa.

Furaha ya shabiki bila furaha ya msanii huo ni msongo wa mawazo, kama ngoma inabamba mtaani msanii hana kitu mfukoni, pia haina maana yoyote.

Twende mbele twende nyuma, Je, Gozdilla kufanya kolabo na Diamond, Alikiba kuna alama yoyote katika muziki wake?, kuna kitu cha kujivunia zaidi ya wimbo husika?. Weka nukta hapo kwa leo.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents