Bongo5 Makala

Makala: Ujio wa Ommy Dimpoz katika Falsafa za Alikiba na Diamond (+Audio)

Usiku wa kuamkia May 02, 2018 msanii Ommy Dimpoz aliweka alama nyingine katika muziki wake kwa kuachia ngoma yake ya pili chini ya label ya ya RockStar4000.

Ngoma aliyoiachia inakwenda kwa jina la Yanje ambayo amemshirikisha mwanadada, Seyi Shay kutoka nchini Nigeria.

Kwanini alama katika muziki wake?: Ommy Dimpoz alisaini RockStar4000 July 6, 2017 na ngoma yake ya kwanza kutoka chini ya label hiyo ni Cheche. Yanje ni ngoma ya pili kutoa na ni ngoma ya kwanza rasmi (official) kwake kufanya kolabo na msanii mkubwa wa nje ukiachilia mbali ile remix ‘Tupogo’ aliyomshirikisha J Martin.

Hivyo ujio huo wa Ommy Dimpoz chini ya RockStar4000 ni mkubwa kuliko ule wa mwanzo na pengine katika vipindi vyote alivyowahi kukaa kimya na kuibuka tena.

Falsafa za Alikiba na Diamond Kivipi

Kwa tafsiri; maana ya neno Falsafa ni jaribio la kuelewa na kueleza ulimwengu kwa kutumia akili inayofuata hoja za mantiki. Huchunguza mambo kama kuweko na kutokuweko, ukweli, ujuzi, uzuri, mema na mabaya nakadhalika.

Hivyo falsafa ni mantiki inayoeleza hatua zake ikiwa tayari kuchunguza upya kila hatua iliyochukua kwa njia ya kuuliza maswali na kutafuta majibu. Weka nukta hapo.

Baada ya Ommy Dimpoz kuachia wimbo wake ‘Yanje’, Alikiba ambaye ni miongoni mwa wamiliki wa RockStar4000 alihaidi wimbo huo ukifikisha views milioni tatu ataachia ngoma mpya, hata hivyo hajaweka wazi ni kwa kipindi gani.

Si mara ya kwanza Alikiba kutoa ahadi inayofanana na hiyo, September 2017 wakati anafanya media tour kwa ajili ya ngoma yake ‘Seduce Me’ aliiambia Bongo5 kuwa ngoma hiyo ikifikisha views Milioni 10 ndani ya mwezi mmoja anatatoa ngoma nyingine.

“Inawezekana, acha tu niwaambie ikifika views Milioni 10 ndani mwezi mmoja kiukweli mimi natoa ngoma nyingine, yaani natoa tena kwa hasira, na deal nayo haraka sana,” alisema Alikiba.

Tangu kipindi hicho hajatoa ngoma yoyote mpya, hii ni kutokana kiasi kile hakikufikiwa kwa muda aliyoutaja. Utakumbuka Alikiba si msanii wa kutoka nyimbo mara kwa mara, hivyo sasa anaishi katika maisha yake ya kila siku ya kimuziki.

Ukisiliza wimbo wa Ommy Dimpoz ametumia lugha tatu ambazo ni Kiswahili, Kinyarwanda na Kingereza. Muimbaji Seyi Shay ameimba lugha ya kiswahili katika wimbo huo.

Huu ni utaratibu ambao wasanii wa Bongo wanaanza kuupalilia katika muziki wao pindi wanapofanya kolabo na wasanii wa nje.

Utakumbuka mwezi mmoja uliyopita Diamond aliachia ngoma inayokwenda kwa jina la African Beauty ambayo amemshirikisha Omario kutoka nchini Marekani.

Katika ngoma hiyo Omario ameimba Kiswahili kwa kiasi kikubwa kitu ambacho kimeifanya kuwa tofauti na ngoma nyingine alizofanya Diamond na wasanii kama Ne-Yo na Rick Ross. Tusimame hapo.

Maswali ya Msingi

Kama nilivyotangulia kueleza; Falsafa ni njia ya kuuliza maswali na kutafuta majibu yake. Katika mambo mawili niliyoeleza kuhusu Diamond na Alikiba, yana maswali yake ambayo tunapaswa kujiuliza na kuyatafutia majibu yake.

Mosi; Kwanini wimbo wa Ommy Dimpoz ufikishe views milioni tatu katika mtandao wa YouTube ndipo Alikiba atoa wimbo?. Pili; kwanini wasanii kama Diamond na Ommy Dimpoz ‘wamewamezesha’ kiswahili wasanii waliowashirisha katika nyimbo zao za hivi karibuni?.

Majibu Yake

Alikiba ni msanii ambaye mashabiki wake wamechizika hasa na muziki wake. Hata hivyo amekuwa na mtindo wa kutokutoa nyimbo kila mara kitu ambacho huwafanya mashabiki wake kuwa na uhitaji zaidi kutoka kwake.

Mashabiki wake wanaposikia yupo mbioni kutoa ngoma lazima wachizike, anakuwa amechokoza hisia zao. Sasa anapowaambia wimbo wa Ommy Dimpoz ukifikisha idadi hiyo ya views atatoa ngoma hapo amenena mambo mawili kwa lugha ya kificho (indirect language)

Mosi; anawafanya kama sio kuwalazimisha mashabiki wake wakaangalie wimbo huo na ku-share kwa lengo la kifikia kiasi hicho cha views ili kupata wimbo mpya kutoka kwake. Kumbuka hapo Ommy Dimpoz atawachukua na mashabiki wa Alikiba.

Pili; hiyo ni mbinu ya kibiashara ambayo ameitumia Alikiba. Yeye akiwa kama miongoni mwa wamiliki wa RockStar4000 angependa kuona msanii aliyechini yake anafanikiwa. Kufanikiwa kwa muziki wa Ommy Dimpoz ni kufanikiwa kwa RockStar4000 kibiashara. Weka nukta hapo.

Jibu la Pili; Bila shaka Diamond ndiye aliyemwandikia Omario mashairi ya kiswahili katika wimbo wake wa African Beauty. Hii ni mbinu ya kuwafanya mashabiki/wasikilizaji kutoboreka aidha kwa kutokujua lugha ya msanii aliyeshirikishwa.

Pia kufanya wimbo husika kuwa na wepesi wa kusikilizika (kwa wale wanaojua kiswahili pekee) ambao ndio wengi. Hivyo Diamond na Ommy Dimpoz wamejiuliza maswali ni kwa namna gani watawashirikisha wasanii wa nje na kufanikiwa katika eneo hilo kisha wakatafuta majibu wake.

Mwisho; Bila kujali ‘timu na siasa’ za kimuziki wasanii wote watatu niliyowazungumzia katika makala hayo, jitihada zao katika kukuza muziki wa Bongo Flava kimataifa zinapaswa kuthaminiwa na yeyote ambaye ni muungwana kimatendo na kimtazamo katika muziki huo.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents