HabariSiasa

Makao Makuu ni Dodoma – Waziri Simbachawene

Serikali imesema haina mpango wa kurejesha Makao Makuu ya nchi Dar es Salaam na kwamba miradi mingi mikubwa inatekelezwa Dodoma kutokana na umuhimu wa Makao Makuu.

Hayo yamesemwa bungeni jijini Dodoma na Waziri Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu George Simbachawene wakati akijibu swali la mbunge wa jimbo la Ukonga mkoani Dar es Salaam, Jerry Silaa aliyetaka kujua ni kwa nini serikali isitenge siku za kutoa huduma kwenye ofisi za Dar es Salaam ili kupunguza gharama za wateja wanaosafiri kufuata huduma Dodoma.

Amesema uamuzi wa serikali kuhamia Dodoma ulikuwepo tangu mwaka 1973 na ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa miaka yote ilielekeza hivyo.

Kwa mujibu wa Waziri Simbachawene, serikali ilishahamia Dodoma na wizara zilipewa shilingi bilioni 20 ili kufanikisha mpango huo.

Aidha Waziri Simbachawene amesema kuna baadhi ya watu ambao wanamsingizia Rais Samia Suluhu Hassan kwamba hapendi kuhamia Dodoma, jambo ambalo si la kweli.

Amesema majengo makubwa ikiwemo Ikulu ya Dodoma yapo katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wake, hivyo wananchi wamuunge mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza shughuli za maendeleo.

“Taasisi zote ambazo bado hazijahamia Dodoma serikali inafanya tathmini na wiki ijayo nitatoa tathmini ya serikali kuendelea kufanya shughuli zake kwa usawa katika mikoa yote kama ilivyo kwa Dodoma” amesema Waziri Simbachawene

Related Articles

Back to top button