Makombora yapiga uwanja wa ndege kusini mwa Kiev

Uwanja wa ndege wa kijeshi wa Ukraine kusini mwa Kyiv umepigwa kwa makombora ya Urusi. Meya wa Vasylkiv amesema shambulio hilo liliharibu njia ya ndege na ghala la mafuta, pamoja na kusababisha milipuko katika chumba cha kuhifadhia risasi.
Video iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii ilionesha moshi mkubwa mweusi ukifuka kutoka kwenye uwanja wa ndege.
Kwingineko nchini Ukraine, mji wa kaskazini uliozingirwa wa Chernihiv umeshuhudia mashambulizi makali ya makombora.
Hakuna huduma ya maji na katika baadhi ya maeneo hakuna umeme.
Bandari ya kusini ya Mykolaiv, ambayo iko kati ya mji unaokaliwa na Urusi wa Kherson na mji wa tatu kwa ukubwa nchini Ukraine, Odessa, pia imeshuhudia mashambulizi zaidi.
Hospitali ya saratani imepigwa na makombora, ingawa ripoti za awali zinaonyesha kuwa haijaharibiwa sana.
Makadirio kutoka kwa maafisa wa ulinzi wa Uingereza ni kwamba vikosi vingi vya Urusi viko pembezoni mwa mji mkuu.
Wasiwasi kutoka kwa wakuu wa jeshi ni kwamba wanajiandaa kufanya mashambulizi makubwa zaidi katika jiji hilo – na watajaribu kuuzingira pia, kama inavyoonekana katika maeneo mengine kote nchini Ukraine.
Haijawa wazi ikiwa vikosi vya Urusi bado vina uwezo wa kufanya hivyo.
Hapa – pamoja na miji mingine – wanakutana na upinzani mkali wanapojaribu kuingia.

Huku ,Wakaazi wa mji wa Melitopol nchini Ukraine wamejitokeza kupinga madai ya kutekwa nyara kwa meya na majeshi ya Urusi.
Maafisa wa Ukraine wamechapisha video wakisema inaomuonesha Ivan Fedorov akiongozwa akiwa amefumbwa macho siku ya Ijumaa.
Katika ujumbe wake, Rais Volodymyr Zelensky uliwashutumu Warusi kwa “kutumia njia mpya ya ugaidi”.
Melitopol, jiji dogo lililo kusini-mashariki mwa Ukraine, lilikuwa mojawapo ya miji ya kwanza iliyoangushwa na Warusi.