Mameneja wazembe Tanesco kuanza kuchukuliwa hatua

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko ameagiza ripoti ya taarifa kila wiki ya Kituo cha Huduma kwa Wateja ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ianze kutolewa kila mwezi ili kufahamu maeneo yenye changamoto ya umeme nchini na kurahisisha watendaji wazembe kuchukuliwa hatua kwenye maeneo hayo.
Dkt. Biteko ametoa agizo hilo wakati wa ziara kwenye kituo hicho cha huduma kwa wateja leo tarehe 4 Aprili, 2024 jijini Dar es Salaam na kutoa maagizo mbalimbali yenye lengo la kuongeza ufanisi wa kituo hicho muhimu kwa wananchi nchini.
“Wateja wote wanaopiga simu kwa sababu mnaletewa matatizo ya wananchi ni lazima mtengeneze kila wiki tupate ripoti ni mkoa gani wanahudumiwa wateja kwa haraka na mkoa upi haupewi huduma kwa haraka ili tuchukue hatua,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Ameagiza kila mkoa nchini uliopo chini ya TANESCO ufanyiwe tathmini kujua umeme umekatika mara ngapi na kufahamu sababu zilizopelekea umeme kukatika katika maeneo hayo ili kama ni uzembe umefanyika Serikali iweze kuchukua hatua haraka.
“Mimi ninafahamu kuna wakati umeme unakatika sio kwa sababu ya matatizo makubwa bali ni kwa matatizo madogo madogo ya kiusimamizi kwenye laini zetu. Unakuta kuna mahali mti umedondoka kwenye njia zetu na unachukua muda mrefu kuondolewa, au mteja amepiga simu anachukua muda kuhudumiwa, tunahitaji hiyo ripoti,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja Tanesco, Martin Mwambene amesema wataendelea kuhakikisha wateja wao wanapata huduma bora na kwa wakati.
“Tumepokea maelekezo ya Waziri na tutakwenda kuyatekeleza kama tulivyoagizwa, ila yapo baadhi ya mambo yamekwishaanza kwa sasa hivi mteja yoyote anaweza kufungua taarifa yake kupitia Call Center upande wa WhatAssp, tumepata namba ambayo ni 180, ndani ya juma hili tutajipanga ili kuona mteja wetu asichajiwe akipiga simu kuomba huduma,” amesema
Hata hivyo amesema kazi kubwa watakayoifanya sasa ni kuziunganisha ofisi za mikoa za Tanesco na kituo chao cha Kutoa huduma kwa wateja kwa njia ya simu ili kuwa na data zinazofanana na kujua wapi kunachangamoto na kuzifanyia kazi kwa wakati.
“Mteja anachotaka ni umeme hivyo anaporipoti tatizo lake anataka kuhudumiwa kwa haraka hivyo kupitia vitengo vyetu tutajipanga vizuri na tutahakikisha tunawafikia wateja kwa wakati,” amesema Mwabene
Written by Janeth Jovin