Habari

Maonesho ya sabasaba mwaka huu kuwa ya kipekee

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) Latifa khamis amesema maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (DITF) maarufu kama ‘Sabasaba yanayotarajia kuanza Juni 28 hadi Julai 13 mwaka huu yatakuwa ya kipekee kwani yatakuwa na mambo mbalimbali

Pia amesema mpaka sasa maandalizi ya maonesho hayo yamekamilika kwa asilimia 79.

Latifa ameyabainisha hayo leo Juni 20, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya maonesho hayo.

“Tantrade kama kawaida inaendelea na maandalizi yake ya maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam ambayo yanatarajiwa kuanza Juni 28 hadi Julai 13, mwaka huu.

“Maonesho ya mwaka huu yatakuwa ya kipekee kwani wananchi wataweza kukata tiketi kupitia mitandao ya simu ambapo tumeshirikiana na Vodacom lakini pia Utamaduni wa kukata tiketi hapa hatutauondoa kwahiyo mtu atachagua akate tiketi kwa kutumia njia gani,” amesema.

Pia amesema kutakuwa na milango ya kielekloniki ambapo wananchi na magari mengine wataweza kuingia kupitia milango hiyo tuliyoiandaa ambayo itapunguza usumbufu na msongamano.

Vilevile amesema kuwa mpaka sasa Nchi 25 zimethibitishwa kushiriki, huku Kampuni za nje 223 na Washiriki wa Ndani 2979.

“Haya ni mafanikio makubwa kwasababu siku bado lakini kampuni nyingi tayari zimethibitisha na hii haijawa kwa bahati mbaya kama mnavyofahamu Rais Dkt . Samia Suluhu Hassan amekuwa akisafiri Nchi mbalimbali kuitangaza Tanzania kwahiyo haya ni matokeo.

“Lakini kama mnavyofahamu maonesho yetu sio ya kawaida watu tu kuja kutembea yana mambo mengi pia ikiwemo kuleta ajira pamoja na kuchochea uchumi wa Nchi yetu,” amefafanua.

Aidha amesema katika Maonesho ya hayo, pia kutakuwa na program tisa (9) a na siku za mataifa saba ambazo zitafanyika kwa siku tofauti tofauti.

“Kutakuwa na Siku ya Taifa ya China, Egypt, Urusi, India, Japan, Korea na nyingine. Pia kutakuwa na onesho la roboti ambazo tayari zimeshaingia na ziko kwenye majaribio.

“Nitoe wito kwa Watanzania wasiache kutembea maonesho haya kwani sisi tunaamini maonesho ni kituo cha fursa zote, hivyo wajitokeze kwa wingi kutembelea,” amesema.

Ameongeza kuwa viingilio havijabadilika ambapo mtoto ni Sh. 1000 na mkubwa ni Sh. 3000.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents