Habari

Marekani yasubiri pendekezo la Urusi kuhusu Ukraine

Rubio amesema rais wa Urusi Vladimir Putin na waziri wake wa mambo ya nje Sergei Lavrov wameashiria watawasilisha masharti yao pengine wiki hii yatakayowaruhusu kuelekea kupata mkataba wa usitishaji mapigano, na mkataba huo utawaruhusu kuingia katika mazungumzo yatakayovifikisha mwisho vita vya Ukraine.

Rubio pia amesema muongozo utakaowasilishwa na Urusi utatoa taswira kamili kuhusu nia halisi ya Warusi.

Rubio alisisitiza kwamba rais wa Urusi Vladimir Putin hajafanikiwa kumshawishi rais wa Marekani Donald Trump kuhusu jambo lolote, lakini pia kwa upande mwingine Urusi haijaashiria kubadili msimamo wake na kuregeza kamba tangu Trump aliporejea madarakani Januari mwaka huu na ahadi ya kuvifikisha mwisho vita vya Ukraine kupitia mdahalo.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema ni wazi kwamba Urusi inajaribu kuvuta muda ili iendelee na vita vyake na kuikalia Ukraine.

Urusi: Marekani ina jukumu muhimu kumaliza vita na Ukraine

Jeanne Shaheen, mwanasiasa wa ngazi ya juu wa chama cha Democratic katika kamati ya baraza la seneti la Marekani inayoshughulikia sera za nje, alimwambia Rubio kwamba hatua ya Putin kukataa kuhudhuria mazungumzo yaliyofanyika mjini Istanbul nchini Uturuki licha ya nia ya rais Zelensky na Trump kukutana naye, inaonesha Putin anaamini ni kwa masilahi ya Urusi kufanya vita nchini Ukraine kwa muda mrefu kadri inavyowezekana.

Umoja wa Ulaya uliridhia jana Jumanne duru ya 17 ya vikwazo dhidi ya Urusi, ukivilenga vyombo 200 vya kile kinachojulikana kama meli za kivuli za Urusi. Rubio amesema rais Trump anapinga vikwazo vipya kwa kuhofia kwamba Urusi inaweza kugoma kukaa katika meza ya mazungumzo.

Ukraine imesema kazi ya kuwahamisha raia kutoka maeneo zaidi ya 200 katika eneo la Sumy karibu na mpaka na Urusi imeanza. Gavana wa kijeshi wa jimbo la Sumy Oleh Hryhorov alisema kufikia sasa watu 52,000 wamepelekwa katika maeneo salama, ikiwa ni asilimia 60 ya wakazi jumla 86,000 wanaotakiwa kuhamishwa.

Mkutano wa nchi za G7 kujadili hali nchini Ukraine

Wakati hayo yakiarifiwa, mawaziri wa fedha wa nchi zilizostawi kiviwanda duniani za G7 wanakutana nchini Kanada kwa mazungumzo yanayojikita katika mzozo wa Ukraine na kuyumba kwa uchumi wa dunia kulikosababishwa na ushuru uliowekwa na rais wa Marekani Donald Trump.

Katika mikutano itakayoendelea hadi kesho Alhamisi viongozi watajadili hali ya uchumi wa dunia na kutafuta msimamo wa pamoja kuhusu suala la Ukraine ambayo inawakilishwa na waziri wake wa fedha Sergii Marchenko.

Waziri wa fedha wa Kanada Francois-Philippe Champagne amewaambia waandishi habari siku ya Jumannne kwamba uwepo wa Ukraine katika mkutano huo unatoa ujumbe mzito kwa ulimwengu kwamba nchi wanachama wa G7 wanaahidi tena kwa dhati kuisaidia Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi.  Akiwa ameandamana na waziri wa fedha wa Ukraine, waziri huyo pia amesema watajadili jinsi ya kuijenga upya Ukraine.

Mkutano huo wa mawaziri wa fedha wa nchi za G7 na magavana wa benki kuu katika jimbo la Alberta, magharibi mwa Kanada unafanyika huku kukiwa na hali ya kukosekana uhakika miongoni mwa nchi za G7 kuelekea Ukraine kufuatia Trump kurejea madarakani.

Rubio: Matumaini ya amani Ukraine ni madogo mno

Nchi za G7 zikiwemo Uingereza, Kanada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan na Marekani, zimeyumbishwa na Trump ambaye ameijongelea Urusi kutaka mashirikiano nayo na kuwawekea ushuru washirika na washidani wake kibiashara.

Waziri wa fedha wa Ukraine amesema atatafuta nafasi katika mkutano huo wa G7 kusisitiza msimamo wa Ukraine kuhusu umuhimu wa shinikizo zaidi dhidi ya Urusi kuhusu suala la Ukraine.

 

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents