Habari

Masauni awataka Polisi kuwachukulia hatua wanaotoa kauli zinazohatarisha usalama wa nchi

Na Janeth Jovin

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amelitaka Jeshi la Polisi nchini kuwachukulia hatua wale wote wanaosababisha kwa vitendo au kwa kauli kuvunja sheria za nchi na kuhatarisha usalama wa Taifa.

Kauli hiyo ya Masauni inakuja ikiwa yamepita masaa machache tangu Kamati Kuu ya halmashauri ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kusini Unguja, kumfuta uanachama Balozi Ali Abeid Karume ambaye ni mtoto wa kwanza wa Rais Zanzibar Hayati Abeid Amani Karume, kutokana na kauli na vitendo vyake kwenda kinyume na maadili ya chama.

Balozi Karume anadaiwa kutoa kauli ambazo zinakidhalilisha Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuwatukana viongozi wakuu hadharani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Julai 8, 2023, Masauni amesema kumekuwa kuna baadhi ya watanzania wameanza kutumia uhuru wa kutoa maoni uliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan vibaya kiasi cha kutoa kauli ambazo zinalenga kuhatarisha usalama, kuvunja sheria za nchi na kulipasua taifa.

Amesema kauli hizo haziwezi kukubalika na haiwezekani watu kutumia uhuru wa kutoa maoni kuvunja sheria za nchi na kusisitiza kuwa wao wanawajibu wa kusimamia sheria hizo.

“Nilitake jeshi la polisi nchini kutowafumbia macho kikundi chochote au mtu anayetoa kauli ambazo zinalengo la kuivuruga nchi na kuhatarisha usalama, ninatoa wito kwa wananchi pia kujiepusha kutumia uhuru huu uliyotolewa kwa nia njema kuvunja sheria za nchi,” amesema Masauni.

Hata hivyo amesema wanaamini kuwa kasi ya maendeleo na mafanikio makubwa ya serikali ya awamu ya sita yaliyotokea kwa muda mfupi, yametokana na dhamira ya dhati ya Rais Samia na hatua mbalimbali anazozichukua.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Hamad Masauni akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam leo.

“Kila mtu ameshehudia juu ya uamuzi wa rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wa kuimarisha uchumi na demokrasia nchini na uhuru wa watu kutoa maoni yao.

“Dhamira ya Rais katika jambo hili ni njema na CCM inafungua milango ya mawazo na ushauri kutoka kwa mtu yeyote kwa sababu kinaamini jambo hilo ni muhimu, hivyo tutaendelea kupokea ushauri, maoni na mawazo kutoka kwa watu mbalimbali,” amesema

Hata hivyo amesema kama kuna chama ambacho kinasifika kwenye ujenzi wa umoja na mshikamano katika nchi huwezi kuacha kuizungumzia CCM kwani ndicho chenye dhamana ya kuongoza serikali ambayo ina jukumu la kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa salama.

“Vyama vingine havina dhamana hiyo bali sisi CCM tunawajibu wa kuhakikisha tunaendelea kudumisha misingi ya umoja na mshikamano, undugu ambaye hatimaye unahakikisha usalama wa nchi,” amesema

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents