Mastaa wa Azam wakosa Bonasi

KUTOLEWA katika Kombe la Shirikisho hatua ya 32 ikiwa ni mara ya kwanza kwa Azam FC, huku ikiwa na nafasi finyu ya kubeba taji la Ligi Kuu msimu huu, kumewafanya mabosi wa klabu hiyo kuitisha kikao cha dharura kilichotoa maazimio mawili na utekelezaji umeanza katika mechi iliyopita ya ligi dhidi ya TZ Prisons Machi 6 na kushinda 4-0.
.
Azimio la kwanza ambalo uongozi wa Azam umeliamua ni kufuta bonasi zote za fedha ambayo ilikuwa inatoa kila timu inapoibuka na ushindi na wakati mwingine hata sare kutegemeana na uzito wa mechi.
.
Lakini baada ya kupoteza mechi ya Kombe la Shirikisho mbele ya Mbeya City kwa penalti 4-2 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1, wachezaji wa Azam hawatawekewa tena zawadi ya fedha katika mechi zilizosalia hadi msimu utakapoisha.
.
Kiwango cha chini ambacho wachezaji wa Azam wamekuwa wakipata kwa ushindi ni Sh10 milioni nacho huwa kwa mechi za kawaida lakini zipo mechi ambazo mabosi wa timu hiyo huweka hadi zaidi ya Sh100 milioni kama mbinu ya kuwapa hamasa mastaa wa kikosi chao lakini kwa sasa wameamua kutofanya hivyo.
.
Azimio la pili ni kupiga panga idadi kubwa ya wachezaji wa kikosi hicho hasa wale ambao wanaonekana kutokuwa na mchango ndani ya timu hiyo hivyo wamepewa mechi saba kupigania hatima zao, chanzo cha ndani kimeeleza. [via Mwananchi]