Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetaka uchunguzi huru ufanyike, kuhusiana na mauaji dhidi ya mwanamke mjamzito, yaliyofanywa na wanaume waliovalia sare za jeshi katika eneo la kaskazini mwa Msumbiji.
Mkanda wa video ulionekana mtandaoni wiki hii, ukiwaonyesha wanaume hao wakimpiga mwanamke waliyemshutumu kuwa muasi, na kisha kummiminia risasi.
Serikali ya Msumbiji imewatuhumu wanamgambo wa kijihadi kwa mauaji hayo ya kinyama. Waziri wa mambo ya ndani wa Msumbiji Amade Miquidade ameapa kuchunguza kisa hicho, akisema lakini kuwa kilifanywa na waasi waliovaa sare za jeshi la serikali, ili kuuhadaa umma.
Amnesty International imesema mkanda huo ni ushahidi wa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaoendeshwa na maafisa wa usalama wa Msumbiji katika jimbo lenye machafuko la Cabo Delgado.