Habari

Mavunde akabidhi uwanja wa michezo wa kisasa Dodoma

▪Ni wa michezo ya Kikapu,pete na wavu

▪Wazazi na wanafunzi wamshukuru kwa ujenzi huo

▪DC Shekimweri ahimiza matumizi ya kiwanja kuimarisha Afya bora na maadili

Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde amekabidhi kwa uongozi wa Shule ya Sekondari Kiwanja cha Ndege kiwanja cha kisasa cha michezo ya mpira wa kikapu,pete na wavu kama sehemu ya kukuza na kuendeleza vipaji vya wanafunzi wa Jijini Dodoma.

Tukio hilo limefanyika katika shule ya sekondari ya Kiwanja cha Ndege jijini Dodoma .

“Namshukuru sana Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa kuboresha miundombinu ya mazingira rafiki ya kusomea kwa shule zetu nyingi ikiwemo Shule ya sekondari Kiwanja cha Ndege.

Katika kuunga mkono jitihada hizi kubwa nimeamua kujenga uwanja huu wa kisasa wa michezo hapa shuleni ili kusaidia kuibua na kuendeleza vipaji vya wanafunzi wa Dodoma”alisema Mavunde

Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma  Alhaj Jabir Shekimweri amempongeza Mbunge Mavunde kwa juhudi kubwa ya kuleta maendeleo Jijini Dodoma na kuwataka wanafunzi kutumia kiwanja kushiriki kwenye michezo ili kujenga Afya bora hali itakayowasaidia kujiepusha na makundi mbalimbali ambayo yataathiri maadili yao na afya.

Akitoa salamu zake,Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Nchini(TBF) Michael Kadebe amepongeza juu ya ujenzi wa kiwanja hicho kwa kuwa inaongeza idadi ya viwanja vya Mpira wa Kikapu Jijini Dodoma na kuahidi kuanzisha kituo cha mafunzo ya vijana MAVUNDE BASKETBALL ACADEMY katika shule hiyo kama njia ya kuwaendeleza wanafunzi katika ushiriki wao kwenye mchezo wa kikapu Jijini Dodoma.

Wakitoa salamu za Shukrani Diwani wa Kata ya Kiwanja cha Ndege Mh. Amos Mbaranga na Mwenyekiti wa Bodi ya Shule Ndg. Bryson Lema wamemshukuru Mbunge Mavunde kwa ujenzi wa kiwanja katika Shule hiyo ambacho kimebadilisha muonekano wa shule hiyo kimazingira na ambacho kitachochea kuwaandaa wanamichezo wa baadaye na tegemeo la Taifa kupitia shule hiyo huku wakiahidi kukitunza kiwanja hicho kwa hali na mali ili kiwafae kizazi cha sasa na kizazi kijacho.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents