Mbunge Lowassa achangia tsh milioni 11 ujenzi wa nyumba za daktari (Picha)

Mbunge wa Monduli, Fredrick Lowassa amechangia Sh11 milioni katika miradi ya maendeleo katika vijiji vya ujenzi wa nyumba ya daktari wa wilaya hiyo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi zake kwa wapiga kura wa jimbo hilo.

Taarifa ya Ofisi ya Mbunge huyo kwa vyombo vya habari, imesema fedha hizo ni kutokana na mchango wa Mbunge aliyetoa zaidi ya Sh6.8 milioni na taasisi ya ECLAT DC iliyotoa Sh5 milioni.

Fredrick ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, alitoa mchango huo jana alipotembelea eneo litakalojengwa nyumba ya daktari wa wilaya.

Pia alitembelea eneo la shule ya Msingi ya Indonyonado iliyoezuliwa paa lake na upepo, pamoja na zahanati ya Kata iliyopo Engutoto kijiji cha Mlimani.

Lowassa amewashukuru wananchi kwa kumchagua kwa asilimia 93 yeye pamoja na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dk John Magufuli.

“Ninawashukuru sana kwa kutuchagua kwa asilimia kubwa mimi pamoja Hayati Magufuli, licha ya kutokea msiba mkubwa wa kitaifa na kumpoteza sasa tunaye Rais Mama Samia Suluhu Hassan,” amenukuliwa Lowassa akisema katika taarifa hiyo.

Lowassa aliyebeba kauli mbiu ya baba yake ya Elimu Elimu Elimu, alimuomba mfadhili huyo kushirikiana na Ofisi ya Mbunge na Ofisi ya Mkurugenzi kusaidia kujenga Shule ya Msingi Endonyonaado ambacho wananchi walijenga madarasa mawili na kupauwa lakini upepo uliezua.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika la ECLAT DC, Peter Toima alimshukuru Lowassa kwa kumkaribisha jimboni kwake na kuahidi kumuunga mkono katika shughuli za maendeleo.

Taarifa hiyo imesema Lowassa alifahamiana na taasisi hiyo baada ya kutembelea makao kakuu yake yaliyopo wilayani Simanjiro mkoani Manyara na ndipo alipowaalika.

“Kwa heshima hiyo na umuhimu wake alionionyesha Mbunge wa Jimbo la Monduli ninamuahidi kumuunga mkono wa dhati, Mbunge naomba nikajiandae kwa kazi hiyo na niaahidi mwezi wa saba ikimpendeza Mwenyenzi Mungu nakuja na wafadhili eneo hili la Indonyonaado,” amenukuliwa akisema Toima katika taarifa hiyo. .

Related Articles

Back to top button