Makala

Mfahamu Mwl. Nyerere na Fikra za Binadamu Wote ni Sawa na Afrika ni Moja! (Video)

April, 13, 1922, alizaliwa Julius Kambarage Nyerere katika familia ya kichifu, akasoma mpaka Ulaya, akapata ajira yenye mshahara mnono, akaiacha na kwenda kupigania Uhuru, Tanganyika tukawa huru, lakina akasema, “Uhuru wetu hauwezi kuwa na maana kama wenzetu bado wanatawaliwa”, akaelekeza nguvu kuikomboa Afrika, Tanzania ikawa kambi ya Wapigania Uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika, Urafiki Jazz wakamtia moyo Mwalimu kwa vibao murua, Afrika  ikawa Huru, Oktoba 99 mwalimu akapumzika kwa amani akiwa maskini wa vitu na mali, lakini tajiri wa watu na utu!

https://youtu.be/ibg8lCnzRlk

Siku ile Nyerere amezaliwa, aliitwa Mugendi yaani ‘Mtembezi’ au tuseme ‘Mzurulaji,’ lakini mizimu hai ya ukoo wao ikalikataa jina hilo na kuwashauri wamuite “Kambarage” jina la Spirit wa Mvua, Wazee wakatii maana walijua nguvu ya jina, ‘Mugendi’ akaitwa Kambarage, akaja na mvua ya Uhuru, ikanyesha Tanganyika na Afrika yote. Mungu wa Afrika alitenda maajabu, Wazungu wakatudanganya tumuite mshenzi, na wakato wao ndo washenzi. Matokeo yake tunaitana majina ya kishenzi na jamii kufurika washenzi wanaomuenzi Nyerere kinafiki. Leo tunazo hadi kamati za fitina ndani ya vyama vyetu na wakati Nyerere alisema unafiki kwake mwiko. Sio poa mjue!

Katika tumbo la Mama Nyerere walizaliwa watoto nane na katika viuno vya baba yake walitoka watoto 25. Mzee alikuwa na wake 22 na michepuko minne tu. Wote aliwahudumia kwa umaridadi! Sijui wazee wa zamani walikula? Imagine! Baba yake Nyerere alioa katika umri wa miaka 47, tena kabinti ka miaka 15 tu halafu akazaliwa Nyerere, Mkombozi wa Afrika. Kumbuka mama Nyerere alikuwa  mke wa tano, kwahiyo yawezekana mzee aliendelea kuoa mpaka miaka 80, maana alikufa na miaka 82!

Halafu wake zake wote waliishi  kijamaa kwenye compound moja tena kwa upendo, furaha na utii na wakati jamaa yako kamke kamoja tu kanamtoa jasho mpaka kwake anapaona pachungu. Anasubiri kakisinzia ndo anarudi kwa kunyatia kama kibaka wa TV na Deki. Akiongezewa tunne si ndo ataikimbia nyumba yake jumla? Jamaa yako bwana! Salute kwenu wazee wa zamani.

Baba yake Nyerere alikuwa Chifu wa Wazanaki lakini hakuwa na jina kubwa kama machifu wengine, yaani Mkwawa, Fundikira, Mangungo na Songea! Sasa sijui jina lake nalo lilichangia? Maana anaitwa Kiwavi! Ndo maana ya Nyerere! Alizaliwa kipindi cha janga la viwavi jeshi. Ilikuwa mwaka 1860. Zamani waliitana majina kulingana na majira uliyozaliwa. Nyanzara alizaliwa wakati wa njaa, Mayila, njiani na Mukiza wakati wa uponyaji! Wewe unaelewa maana ya jina lako? Ujue ulinge!

Hata hivyo Mzee Burrito Nyerere kupata uchifu ilikuwa ni mpango wa Mungu Afrika tukombolewe. Maana uchifu wake ndo ulimpa Nyerere fursa ya kupata elimu nzuri. Mkoloni alianzisha shule za watoto wa machifu ili waendeleze uchifu kuliko kusomesha majitu nje ya system yakaleta shida. Siunajua tena maskini akitokamo, wanasumbua hao. Hata hivyo pamoja na kumsomesha Nyerere mpaka Ulaya, wakamuongezea na PhD ya heshima bado hakukubali kuwa kibaraka wao kama viongozi wengine. Walimsomesha Mandela akawalinda, walisomesha Kenyatta akawalinda, walisomesha Lumumba akawapinga wakamuua, walimsomesha Kamuzu Banda akawalinda, walimsomesha Mugabe akawageuka wakamuita kichaa, walimsomesha Kwame Nkrumah akawawageuka wakampindua. Sasa hivi Mchina anasomesha vijana wetu kwa kasi, sijui nao wakimgeuka atawaua? Maana hawa ndo viongozi wa Kesho! Sijui usalama wa mali zetu utakuaje! Mungu aingilie tu!

Nyerere alilelewa katika mila na desturi za wazanaki, akachonga meno, akachunga mbuzi na ng’ombe lakini hakuwa ng’ombe, maana maamuzi ya waliochunga yanashangaza. Labda kwa kuwa walizoea kumpiga ng’ombe wa nyuma kwa kosa la ng’ombe wa mbele kuchelewesha mwendo. Nyerere hakuwa hivyo, tangu shuleni mpaka Ikulu alijipa muda wa kufikiri kabla ya kutenda. Muulize Tuntemeke Sanga wa Makete atakusimulia.

Nyerere alitafutiwa mke mapemaaa, kabinti ka miaka minne, akakatosa kiana. Kaliitwa Magori Watiha. Hata alivyoanza kazi pale Tabora walikapeleka kakasomee shule yam singe kule, lakini Nyerere akakapeleka kwa mama yake Mwitongo.  Nadhani ni kwa sababu dini ilimkaa sana. Nyerere alipenda sana kusali. Alitembea maili nne kila siku kwenda kujifunza neno. Lakini kanda maalum raha sana, unazaliwa tu na kuandaliwa mke. Unaweza kuparamia kabinti kumbe ni mali ya mtu.

Nyerere alipenda kula sana mtama kwa sababu mtama una nguvu ya asili walisema wahenga. Hata Kinjekitile aliutumia kuwatia msukosuko wajerumani kwenye ile vita ya maji maji. Kuleni mtama wajukuu zangu ili mpate nguvu za kuishi vyema na wake zenu daima. Pigeni uji wa mtama asubuhi, ugali wa mtama mchana, vitumbua vya mtama jioni na pombe ya mtama usiku mtaniambia.

Huyu Nyerere huyu mwenye jina kubwa Tanzania, Afrika na Duniani kote alibarikiwa akili nyingi za darasani na maishani. Darasani aliwashangaza walimu kwa uwezo wa kujibu maswali kwa haraka na umaridani mkubwa hadi kumrusha darasa. Alitembea umbali wa maili 25 kuifuata elimu. Alianza shule ana miaka 14 labda ndo maana alijielewa. Ilikuwa mwaka 1934. Shuleni hakuwa na muda na michezo. Yeye alikwenda kusoma na akasoma kweli. Hakuwa na mambo mengi kama wanafunzi wa siku hizi. Wana mambo mengi haoo…kama unga wa ngano ati. Mapenzi wao, michezo wao, utoro wao, wizi wa mitihani wao, uvuvi wao, loh! Au ni kwa sababu tunawapeleka shule wakiwa wadogo? Enzi zetu la kwanza ulianza na miaka 15, unamaliza la saba na uwezo wa kutunza mke kabisa. Siku hizi la saba bado ni mtoto kabisa. Sijui tumekosea wapi.

Bidii ya Nyerere katika masomi ilimg’arisha ndani na nje ya nchi. Mwaka 1936 alivyohitimu Shule ya Msingi Mwisenge aliongoza kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi katika mtihani wa taifa. Serikali ya Mkoloni ikampa ufadhili wa kwenda Tabora Boys, huko nako akapiga na kwenda zake Makerere Uganda. Makerere aliingia 1943. Huko ndiko Falsafa na Mitazamo ya Nyerere kuhusu binadamu wote ni sawa ilikoanza kuonekana. Hata kazi alizosoma zilirelate na fikra zake. Alimsoma sana John Stuart Mill. Huyu John Mill ndiye aliyesema kabla hujafanya maamuzi yoyote zingatia matokeo yatakayozalisha furaha kubwa kwa watu wengi. Nyerere alimuelewa sana huyu mshikaji na kuziishi fikra zake. Fikra hizi ndo zilimsukuma Nyerere kuacha mshahara mnono na mke wake na kwenda kupigania uhuru Tanganyika ili kuwafurahisha wengi.

Lakini pia Nyerere hakuwa mtu wa tamaa ya mali na vitu, bali watu na utu. Nasikia hata serikali ilipotaka kumjengea nyumba aliwashushua na kuwaambia jumba lote la nini kwani mie tembo?  Siku hizi kingozi anamiliki nyumba kila mkoa, halafu ni kubwa mpaka bombadia inaweza kupaki. Yaani hapa tunamdhalilisha Nyerere.

Pamoja na kusoma kwake hadi Ulaya hakudharau tamaduni za kwao kama Ocolo, yule mume wa Lawino aliyerudi Afrika na mishauo hadi kero. Wanawake wote wasiovaa mawigi aliwaita washamba, wanaokula kwa mikono badala ya vijiko aliwaita primitive na wasiokwenda disko aliwashangaa sana. Ocolo alikuwa limbukeni, Nyerere alikuwa muungwana. Unyenyekevu wake ulimvutia kila mtu kutaka kufanya naye kazi.

Halafu tangu shule ya msingi mpaka chuo kikuu kule Scotland, Nyerere alipinga unyonyaji na ubepari kwa dhati. Akiwa shule ya msingi alipambana na Herman Abdallah, mkuu wa shule baada ya kula fedha za wanafunzi. Aliadhibiwa kwa utovu wa nidhamu lakini ujumbe ulifika. Akiwa Makerere alindika barua kwa mhariri wa gazeti la Tanganyika Standard kulaani ubepari. Katika Barua hiyo iliyochapishwa Julai 1943 alisema ni vigumu sana kupractice ubepari Afrika kwa sababu waafrika ni wajamaa kwa asili. Lakini pia mwaka 1951, wakiwa Scotland yeye na John Keto waliandika makala kwenye gazeti la chuo kupinga mpango wa mkoloni kuingiza Tanganyika katika shirikisho la Rhodesia na Nyasaland.

Huyu John Keto alikuwa mwanasiasa mzuri sema alijikita sana kwenye ualimu akabaki kuwa daraja la wengine. Hilo ndo balaa la ualimu hapa Dunia. Kamfundisha John Malecela, Paul Rupia, David Wakati, Jackson Makweta, Horace Kolimba, Julius Sepeku pale Minaki. Alifariki 26 Desemba 2012 akiwa na umri wa miaka 95. Alizikwa kwao Tanga.

Alipinga pia unyanyasaji wa kijinsia kwa kuandika insha akionyesha application ya falsafa za Mills katika haki za wanawake. Mara nyingi aliwachallenge wanawake kama wanataka kuondoa unyanyasaji wa kijinsia basi waanze na kupinga mahari. Katika hilo hakueleweka kabisa ndo maana mahari zinaendelea!

Pamoja na harakati zote hizo, hakumsahau mama yake mjane. Hata siku ile ametoka Makerere break ya kwanza ilikuwa kwa mama yake, akamjengea nyumba.Kitendo hiki kilimrariji sana mama yeke aliyeachwa na mume wake mpenzi . Mumewe alifariki Machi 1942 Nyerere akiwa mwaka wa mwisho pale Tabora Boys na alinyimwa ruhusa ya kuhudhuria mazishi.

Baada ya kumjengea nyuba mama yake Nyerere alirudi kufundisha zake Milambo Sec, enzi hizo ikiitwa Mt. Maria. Milambo shule ya vijana watukutu kweli. Nakumbuka tukiwa pale tulijiita Milambo Men na Taabora School tukawaita Tabora Wavulana. Halafu Tabora Girls madem zetu. Ujinga mtupu!

Nyerere akiwa Tabora, alijiunga na TAA. Alichaguliwa kuwa mweka hazina wa chama kwa sababu hakuwa mwizi.Alikuwa na kina Chifu Fundikira. Wakafungua Duka la Ushirika na kuuza  mahitaji madogo madogo kama sukari, unga na sabuni. Aprili 1946 alhudhuria mkutanao wa TAA Dar es Salaam, mkutano uliotangaza rasmi kuangia kwenye harakati za kupigania Uhuru.

Hata hivyo mwaka 1949 kwa ushauri wa Fr Richard Walsh, Mkuu wa Shule, Nyerere alikwenda Scotland kwa masomo ya juu. Alipiga Master of Arts Degree pale University of Edinburgh. Aliwaza sana angemuachaje mama yake lakini akapiga moyo konde, akaenda Ulaya kwa sababu safari siyo kifo. Ulaya alipiga vibarua mashambani kujiongezea kipato na kusupport familia yake.

Nyerere alimaliza masomo yake Ulaya na Oktoba 1952 alirejea nyumbani, akajenga  kijumba pale Musoma, kisha akafunga ndoa mpenzi wake Maria Gabriel, kutoka kabila tofauti. Ilikuwa 24 Januari 1953. Alioa kabila lingine kwa sababu hakuamini katika ukabila. After all Afrika hatukuwa na ukabila, tulikuwa na koo. Ukabila uliletewa na wakoloni kutugawa.

Baada ya ndoa Nyerere walihamia Pugu, St Francis’ College, alikoajiriwa kwa kazi ya ualimu. Mwaka 1953 wakabarikiwa mtoto wa kiume, wakamuita Andrew Burrito na kufatiwa na Anna Watiku, Anselm Magige, John Guido, Charles Makongoro, Godfrey Madaraka, Rosemary Huria na Pauleta Nyabanane. John tu ndo alifariki. Hakuna mtoto wa Nyerere aliyefia kwenye ndege kipindi za Vita vya Kagera kama ulivyokuwa unajua. Sijui ulizitoa wapi habari za uongo. Nakushangaa sana ujue!

April 1953, Nyerere alichaguliwa kuwa Rais wa TAA, kutokana na  umahiri wake wa kuongea na kujenga hoja. Julai 7, 1954 TAA ilibadilishwa na kuwa  TANU. Historia ya TAA ni ndefu pia. Nitakuelezea wakati ukifika.

Agost 1954, Umoja wa Mataifa ulipendekeza Tanganyika kupata Uhuru miaka 25 ijayo. Wazee wakasema acheni utoto. Wakamtuma Kambarage kwenda UNO kupinga hoja kwa hoja! John Rupia ndo alilipa nauli. Alikuwa na mawe usipime. March 1955, Nyerere akatinga UNO. Akajenga hoja za utayari wa kujitawala mpaka UNO yote ikalegea.

Mwingereza naye tumbo joto, kunyang’anywa kitumbua na Mzanaki. Mkoloni akashinikiza Kanisa limfukuza kazi Nyerere asijeleta vurugu kama Mau Mau. Kanisa ndo lilimuajiru. likamwambia achague siasa au kazi. Nyerere akachagua siasa. “Mpendwa Fr. Lynch, tayari nimezingatia chaguo ulilonipatia, kati ya ajira yangu shuleni na uanachama wa TANU , na nimefikia uamuzi kwamba ni lazima nijiudhuru kazi yangu ya kufundisha,” aliandika Nyerere katika Barua yake ya 22 Mach 1955. Ujasiri huu ni zaidi ya ule wa kuhonga mshahara mzima.

April 1955 Nyerere akamrudisha mke wake kijijini Butiama, Mwitongo na Oktoba 1955 akarudi Dar es Salaam tayari kwa mashambulizi ya uhuru. Alizunguka nchi nzima akihubiri uhuru. Alitumia Landrover la TANU. Mikutano ya Nyerere ilikuwa amsha amsha! Watu walifurika utadhani mechi ya Simba na Yanga. Alihamasisha matumizi ya amani badala ya nguvu katika kupigania Uhuru na watu walimtii. Alimuiga Mahtma Ghandi, yule mpigania Uhuru wa India aliyeamini amani haiji kwa ncha ya mkuki na makali. Namkubali sana huyu jomba!

Upepo wa Nyerere ulimsumbua sana Edward Twining, Gavana wa Tanganyika hadi na yeye akaanzisha chama cha United Tanganyika Party (UTP) ili kupambana na TANU. Twining alimtuhumu Nyerere kwamba anahubiri ubaguzi nchini. Nyerere akasema, tunapambana dhidi ya ukoloni na siyo wazungu. Wazungu walifanya mengi mazuri tatizo lao yaliwanufaisha wachache. Nchi ilikuwa na shule bora kabisa, wakasoma wao, hospitali nzuri wakatibiwa wao. Huo ndio ukoloni alioukataa Nyerere ingawa unarudi tena kwa kasi.

Leo mtu anaheshimika kwa pesa na si utu. Sasa tunabaguana kuanzia mtaani hadi shule, misikitini hadi kwenye madhababuhi, hospitali mpaka baa! Tunafundishwa kwa mitaala ya Cambrige na mitala inayozalisha wasomi huru gerezani. Si rahisi sana mtoto wa waziri, mzungu, muhindi, balozi na mwarabu huko kwenye mitaala ya elimu bure. Labda mwarabu koko.

Hayo ndo Nyerere aliyapinga mpaka kuwaita wakoloni mashetani na maharamia wakamshitaki na kumpiga faini. Aliwatukana kupitia gazeti lake la SAUTI YA TANU mwaka 1958. Alipigwa faini ya Sh 3,000. Akazilipa, Bibi Tit Mohammed na wanawake wanzake wakafurahi mzee kukwepa kifungo. Walipitia changamoto nyingi wakati wa kupigania uhuru. Kuna wakati walizinguana wao kwa wao, siku nyingine mkoloni akawazingu, tutayaangalia haya katika sehemu ya pili!

Usinichoshe, nisikuchoshe, tusichoshane!

By Denis Mpagaze

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents