Habari

Mfasiri wa FBI afunga ndoa na muajiri wa IS aliyekua akimchunguza

Shirika la ujasusi nchini Marekani FBI limethibitisha kuwa mmoja wa wafasiri wake alifunga ndoa na mwajiri wa Islamic State ambaye alikuwa akimchunguza.

Shirika hilo la kijasusi lilichukua hatua katika maeneo kadhaa ili kubaini na kuimarisha usalama baada ya kisa hicho, FBI iliambia chanzo cha habari cha BBC.

Daniela Greene aliwadanganya waajiri wake kuhusu ziara ya 2014 kulingana na chombo cha habari cha CNN ambacho kilifichua habari hiyo.

Danieal mwenye umri wa miaka 38 alihudumia kifungo cha miaka miwili jela baada ya kurudi nchini Marekani.
Habari hiyo ya Green ilipangwa kuwa ya siri na Jaji mmoja wa Marekani lakini ikafichuliwa kwa mara ya kwanza siku ya Jumatatu baada ya rekodi za mahakama ya jimbo kufunguliwa.

Mtu ambaye Green alifunga ndoa naye ni Denis Cuspert ambaye ni raia wa Ujerumani aliyebadilika na kuwa mwajiri wa Islamic State.Mnamo mwezi Februari 2015, serikali ya Marekani ilimtaja kuwa gaidi duniani. Katika video moja ya Propaganda alionekana akishikilia kichwa cha mtu kilichokatwa.

Green ambaye alihudumu katika afisi ya Detroit alipewa kazi ya kumchunguza Cuspert kulingana na CNN. Miezi sita baadaye mfasiri huyo wa lugha ya Ujerumani alielekea nchini Syria kufunga ndoa naye.

Greene aliyezaliwa nchini Czechoslovakia aliambia wakubwa wake alikuwa anapanga ziara ya kuwatembelea wazazi wake nchini Ujerumani. Lakini badala yake akasafiri kuelekea Uturuki ambapo alivuka mpaka wa Syria kwa usaidizi wa wahudumu wa Islamic state, CNN ilisema.

Wakati huo Greene alikuwa bado ameolewa na mwanajeshi mmoja wa Marekani. Muda mfupi baada ya kuwasili nchini Syria mnamo mwezi Juni 2014, aliripotiwa kufunga ndoa na Cuspert. Alikua amewacha jina lake la usanii Deso Dogg na kujiita Abu Talha al-Almani.
Lakini Greene alikuwa na mafakira mengine kuhusu mumewe wa pili. Kulingana na CNN alimwandikia mtu mmoja ambaye hakutajwa nchini Marekani :”Nadhani nimefanya kitu kibaya wakati huu”.

Siku ya pili aliongezea: ”Nipo katika mazingira hatari sana na sijui nitakuwa hapa kwa muda gani,lakini haijalishi, najuta”.

Denis Cuspert
Mwezi mmoja baada ya kuwasili Syria aliitoroka nchi hiyo na kurudi nchini Marekani. Alikiri kwa wachunguzi kwamba alimwambia Cuspert kwamba anachunguzwa na FBI ,kulingana na ripoti hiyo ya CNN.
Haijulikani ni vipi alifanikiwa kulitoroka eneo hilo la IS .

Greene alikiri makosa hayo mnamo mwezi Disemba 2014 kwa kudanganya kuhusu ugaidi wa kimataifa. Alihudumia kifungo cha miaka miwili jela na aliwachiliwa mwaka uliopita. Green kwa sasa anafanya kazi kama muhudumu anayewakaribisha wageni katika hoteli moja ambayo haikutajwa.

Chanzo BBC.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents