Miji ya Ulaya inayogawa kuku bure kwa wananchi

Miji nchini Ufaransa na Ubelgiji imekuwa ikitoa kuku bure kwa miaka mingi ili kukabiliana na upotevu wa chakula. Karibu na Pasaka mwaka 2015, mji wa Ufaransa wa Colmar ulianza kutoa kuku bure kwa wakaazi wake.
Lengo la mpango huu uliokuwa wa majaribio, uliozinduliwa na idara ya ukusanyaji taka katika mji wa kaskazini mashariki mwa Ufaransa, ilikuwa kupunguza upotevu wa chakula.
Mradi huo umefanya kazi. Meya wa wakati huo wa mji wa Colmar AgglomĂ©ration, Gilbert Meyer, alikuwa amechaguliwa tena mwaka 2014 chini ya kauli mbiu “familia moja, kuku mmoja.”
Mwaka uliofuata operesheni hiyo ilianzishwa, kwa ushirikiano na mashamba mawili ya ufugaji kuku yaliyo karibu. Zaidi ya nyumba 200 katika maanispaa nne zilijiandikisha na kupewa kuku wawili kila moja.
Kila kaya ilitia saini ahadi ya ufugaji wa kuku, kwa maelewano kwamba idara ya taka inaweza kufanya ukaguzi wa maeneo ya kuku hao wakati wowote. Vibanda vya kuku havikutolewa, ilikuwa juu ya wakazi kujenga au kununua. Idara ilihakikisha kila kibanda kina nafasi ya kutosha kwa kuku – kati ya 8 na 10 sq m (86 na 108 sq ft).
“Mpango huo ulifanikiwa – na bado unaendelea. Manispaa nyingine zilijiunga na mpango huo 2022. Na kwa sasa manispaa zote 20 za mji huo zinashiriki,” anasema Eric Straumann, meya wa sasa wa Colmar AgglomĂ©ration.
Kufikia sasa, kuku 5,282 wamesambazwa kwa wakazi wa eneo hilo, na maombi yamefunguliwa kwa awamu inayofuata ya usambazaji kuku kuanzia Juni 2025. Sio tu kwamba wakazi wamepata mayai ya bure, pia taka za chakula zimepungua katika dampo kwani kuku wanalishwa mabaki ya jikoni ya chakula ambayo yangetupwa.
“Kuku ana wastani wa umri wa kuishi wa miaka minne na hula kwa wastani wa gramu 150 (5.3oz) kwa siku, tunakadiria kuwa tumeepuka tani 273.35 za takataka [tangu 2015],” anasema Straumann.