Habari

Milioni 686 kutumika kukamilisha Stendi ya mabasi Lundusi Songea, wakazi zaidi ya 2,000 kunufaika

Chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, mradi wa ujenzi wa Stendi ya Kisasa ya Mabasi Lundusi katika Wilaya ya Songea, Mkoa wa Ruvuma, unaotekelezwa kwa ufadhili wa TASAF kwa gharama ya takribani Sh. Milioni 686, umeanza Agosti 2023 na kufikia zaidi ya asilimia 78 ya utekelezaji, ukitarajiwa kukamilika Januari 2025 na kuanza kufanya kazi saa 24.

Stendi hii, iliyoko kilomita 45 kutoka Songea Mjini na kilomita 20 kutoka Peramiho, inalenga kutatua changamoto ya muda mrefu ya wakazi wa Lundusi na vijiji jirani waliokuwa wakilazimika kusafiri mbali hadi Songea kupata huduma za usafiri wa mikoani, hali iliyowalazimisha kutumia gharama kubwa za usafiri wa bodaboda, malazi na chakula.

Mradi huu tayari umezalisha zaidi ya ajira 300 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, na unatarajiwa kuwanufaisha wakazi zaidi ya 2,000 kwa kutoa fursa za biashara ndogo ndogo, hasa kwa vijana na wanawake, pamoja na kuongeza kipato kwa waendesha bajaji, bodaboda na wauzaji wa vyakula na matunda.

Stendi hii itakapokamilika itakuwa na eneo la kuegesha mabasi, maduka 36 ya biashara ndogo, vyoo vya umma, jengo la utawala na jengo la walinzi wa usalama, hivyo kubadilisha mazingira ya kiuchumi na kijamii ya wakazi wa Lundusi kwa kuleta huduma karibu na makazi yao na kupunguza gharama za maisha.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents