Miloud Hamdi awagawanya Mabosi Yanga

Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi baada ya kutwaa makombe matatu amewagawa mabosi wa klabu hiyo na sasa wameanza kufikiria kumpa mkataba mpya tofauti na ilivyokuwa awali.

.
Hamdi ambaye alianza kuitumikia Yanga, Februari 2025, akitokea Singida Black Stars baada ya kocha wa kikosi hicho Sead Ramovic kuondoka, alipewa mkataba wa miezi sita na alitakiwa baada ya msimu kumalizika aachane na timu hiyo, lakini baada ya mafanikio makubwa mabosi wa timu hiyo wanafikiria kumpa mkataba mpya.
.
Kocha huyo amefanikiwa kuipa Yanga makombe matatu yaani Ligi Kuu, Kombe la Muungano na Kombe la Shirikisho (FA) ambalo Yanga imelitwaa majuzi Zanzibar kwa kuichapa Singida Black Stars mabao 2-0 katika mechi ya fainali.

.
Pamoja na kuwapo kwa kipindi kifupi, lakini anatajwa kuwa mmoja kati ya makocha ambao wamepata mafanikio makubwa zaidi kwenye kikosi cha Yanga.
.
Taarifa ambazo nimezipata kutoka chanzo cha uhakika ndani ya timu hiyo zinaeleza kuwa matokeo mazuri ambayo ameyapata yanawasukuma mabosi wa timu hiyo kuwa na vikao mbalimbali ili kujadili kuhusu uwezekano wa kumpa mkataba mpya kabla hajaondoka kwenda mapumzikoni

.
“Mechi za mwisho Yanga imekuwa inacheza soka kubwa na mabosi wanabishana wampe mkataba mrefu zaidi au waendelee na mchakato wa kutafuta kocha mpya mchakato ambao ulishaanza. wanaotaka abaki wanaonekana kuwa na hoja kuwa amekaa muda mfupi, lakini ameivusha Yanga sehemu ngumu na kuipa mataji,” chanzo kinasema
.
Mmoja wa viongozi wa klabu hiyo amefunguka kuwa: “Unajua kadri muda unavyosogea tumekuwa tunaona utofauti. Timu inacheza kwa mbinu hasa pale kati na tunavyo jenga mashambulizi na hata tunavyoshambulia.
.
“Kuna umakini mdogo tu ukiongezeka tunaweza kushinda kwa idadi kubwa ya mabao… kwa ambayo tunayakosa huwezi kusema ni tatizo la benchi la ufundi ni utulivu wa wachezaji wenyewe, sasa wapo wanaona tuvute subira kwanza ukizingatia tumebadilisha sana makocha msimu huu.