Habari

Mkurugenzi Kampuni ya Udalali ya Yono atunukiwa Shahada ya Uzamivu, ataka jamii kupinga ukatili wa kijinsia

Mkurugenzi wa Kampuni ya Udalali ya Yono, Scholastica Kevela ametunukiwa Shahada ya Uzamivu katika masuala ya fedha (PhD in Finance) na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) huku akisisitiza jamii kuendelea kupinga ukatili wa kijinsia hasa kwa watoto na wanawake.

Dk. Kevela ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT) mkoa wa Njombe, amesisitiza pia atatumia elimu hiyo aliyoipata kuhakikisha anawasaidia wanawake kujikwamua kiuchumi.

Dk. Kevela ametunukiwa PhD hiyo Desemba 5,2024 na Waziri Mkuu Mstaafu na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria, Mizengo Pinda, wakati wa mahafali ya 43 yaliyofanyika mkoani Kigoma.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kumpongeza Dk. Kevela amesema wazazi wote nchini wanapaswa kuwalea watoto kwa usawa bila ubaguzi ili kuepuka vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Amesema ni muhimu Jamii kupinga kwa nguvu zote ukatili wa kijinsia wa aina zote ili kufikia malengo ya kuwa na kizazi chenye usawa Kati ya wanawake na wanaume.

“Ukatili wa kijinsia ni moja Kati ya vitu vinavyosababisha ndoto za watu wengi hususani wanawake na watoto kushindwa kutimia hivyo ni muhimu jamii ikaachana na vitendo hivi vya ukatili, amesema Dk. Kevela

Aidha Dk. Kevela amesema kuwa atatumia elimu aliyoipata kuhakikisha anawakomboa wanawake kiuchumi hasa walioko vijijini.

“Nimesoma PhD katika utu uzima, nimejifunza mengi na nimefanya utafiti wangu katika Mkoa wa Njombe kuangalia namna gani kinamama wa Mkoa wa Njombe watanufaika kiuchumi, kisiasa na kijamii kupitia taasisi za fedha, nimeangalia zinawasaidiaje kinamama wanaoongoza kaya vijijini.

“Tungetamani kupitia ‘microfinance institution’ kinamama wawezeshwe kunufaika kiuchumi, mama awe na uwezo wa kumiliki nyumba, kusomesha watoto, ninachowaambia Watanzania hakuna kukata tamaa, watoto wetu, wanawake tunatakiwa tukaze buti,” amesema Dk. Kevela.

Ameishauri Serikali kuzitupia macho taasisi za fedha hasa zile zilizoko vijijini ambako ndiko kuna Watanzania wengi kwa kuhakikisha wanaongeza mitaji ili waweze kukopa mikopo mikubwa itakayowafaa maishani mwao.

Dk. Kevela pia amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi bora na kwa kuweka mazingira mazuri ya elimu ambayo yamewasaidia Watanzania wengi kujiendeleza kielimu.

“Tunamtazama Dk. Samia Suluhu kama ‘Roll model’ wetu, niwahamasishe vijana wa Tanzania na kinamama wenzangu twende darasani, elimu inasaidia kukuza uelewa. Chuo Kikuu Huria ni rafiki, unaweza kusoma ukiwa unaendelea na majukumu mengine,” amesema Dk. Kevela.

Mgeni rasmi katika mahafali hayo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Watanzania wanayo matumaini makubwa kwa wahitimu wa ngazi mbalimbali katika chuo hicho kwa kuwa ndiyo chachu katika maendeleo ya nchi.

Written Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents