Habari

Mkuu wa jeshi la majini, Schoenbach ajiuzulu Ujerumani 

Mkuu wa jeshi la wanamaji nchini Ujerumani Kay-Achim Schoenbach amejiuzulu baada ya kutoa matamshi yenye utata kuhusu mzozo wa Ukraine.

Deutschland Kay-Achim Schönbach

Schoenbach amejiuzulu Jumamosi usiku baada ya kusema kwamba Rais wa Urusi, Vladmir Putin anahitaji heshima na kwamba Rasi ya Crimea kamwe haitorejea kwa Ukraine.

“Anachohitaji sana ni heshima. Na kumpa mtu heshima ni gharama ndogo. Iwapo ingeulizwa, ni rahisi kumpa heshima anayoidai na pengine anastahili heshima hiyo,” alifafanua Schoenbach.

Ukraine yamuita balozi wa Ujerumani

Schönbach aliyatoa matamshi hayo siku ya Ijumaa akiwa ziarani nchini India, ambayo hayakuifurahisha Ukraine na kusababisha wizara yake ya mambo ya nje kumuita balozi wa Ujerumani, Anka Feldhusen kuelezea kwamba haikubaliani na matamshi hayo.

Schoenbach amesema amemuomba Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Christine Lambrecht kumruhusu aachane na majukumu yake mara moja na amethibitisha kuwa waziri huyo amelikubali ombi lake.

Matamshi hayo ameyatoa baada ya Urusi kuwapeleka wanajeshi 100,000 katika mpaka wake na Ukraine na kusababisha wiki kadhaa za mazungumzo ya kidiplomasia kuzuia uhasama kuzuka.

Ukraine Konflikt Soldaten Territorial Defense ForcesWanajeshi wa Ukraine wakiwa katika mafunzo mjini Kyiv

Hata hivyo, Urusi imekanusha kuivamia Ukraine kijeshi, lakini imetaka kuhakikishiwa na Jumuia ya Kujihami ya NATO kuwa haitoingia kwenye ardhi ya Ukraine, wala haitoendelea kujitanua katika upande wa mashariki ya Ulaya.

Akizungumza katika Taasisi ya Mafunzo ya Ulinzi na Utafiti ya Manohar Parrikar, Schoenbach alisema anaiona China kuwa ndiyo kitisho kikubwa na kwamba Ujerumani na India kwa pamoja zinamuhitaji Urusi kwa lengo la kupambana na China.

Kuhusu mzozo kati ya Urusi na Ukraine, Schoenbach amesema Rasi ya Crimea imetoweka na ukweli ni kwamba haiwezi kamwe kurejea Ukraine. Matamshi yake yanagusia hatua ya Urusi kuinyakua Rasi ya Crimea mwaka 2014, moja ya matukio yaliyoanzisha uhasama uliodumu kwa muda mrefu.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Ujerumani amesema wizara hiyo imejitenga na maoni ya Schoenbach na kwamba matamshi hayo hayafungamani na msimamo wa wizara.

Schoenbach anapaswa kujieleza

Wizara hiyo imesema Schoenbach anapaswa kujieleza kwa mkuu wake, Inspekta Jenerali Eberhard Zorn na kwamba serikali ya muungano ya Ujerumani italijadili suala hilo siku ya Jumatatu.

Kwa upande wake Schoenbach ameomba radhi kupitia ukurasa wake wa Twitter, akisema matamshi yake yalikuwa “kosa la wazi,” na hakuna haja ya kubishana. “Matamshi yangu ya sera ya utetezi wakati wa kikao na taasisi ya India yaliakisi maoni yangu binafsi kwa wakatu huo,” aliandika Schoenbach. Amesema matamshi yake hayaakisi msimamo wa wizara ya ulinzi.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba ameikosoa hatua ya Ujerumani kukataa kupeleka silaha nchini humo na kuitaka Ujerumani kuacha “kuudhofisha umoja” na “kumuhimiza Rais Putin, huku kukiwa na hofu ya Urusi kuivamia Ukraine.

Strategischer Dialog zwischen USA und UkraineWaziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba

Wito wa Ukraine kwa nchi washirika wa Magharibi kuimarisha uwezo wake wa ulinzi umeshuhudia Marekani, Uingereza na mataifa ya Baltic yamekubali kupeleka silaha Ukraine, zikiwemo za kujikinga na mashambulizi ya vifaru vya kijeshi.

Mapema Jumamosi Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Christine Lambrecht alisema nchi hiyo haina mpango wa kuipatia silaha Ukraine katika mzozo unaondelea kati yake na Urusi. Hata hivyo alisema serikali ya Ujerumani itaendelea kuiunga mkono nchi hiyo dhidi ya kitisho kutoka Urusi.

Kuleba aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba kauli ya Ujerumani kuhusu kutoweza kuipatia silaha za ulinzi Ukraine, hazilingani na hali ya sasa ya kiusalama.

Related Articles

Back to top button