HabariMakalaMichezo

Mo Farah afichua siri kusafirishwa kinyume cha sheria kwenda Uingereza, ataja jina lake halisi

Sir Mo Farah alipelekwa nchini Uingereza kinyume cha sheria akiwa mtoto na kulazimishwa kufanya kazi kama mtumishi wa nyumbani, amefichua.

Nyota huyo wa Olimpiki ameiambia BBC kuwa alipewa jina la Mohamed Farah na wale waliomsafirisha kutoka Djibouti.

Jina lake halisi ni Hussein Abdi Kahin. Alisafirishwa kwa ndege kutoka nchi hiyo ya Afrika Mashariki akiwa na umri wa miaka tisa na mwanamke ambaye hajawahi kukutana naye, na kisha kulazimishwa kuwatunza watoto wa familia nyingine, anasema.

“Kwa miaka niliendelea kujizuia kuzungumza,” mwanariadha wa Timu ya GB anasema. “Lakini unaweza tu kuizuia kwa muda mrefu.” Mwanariadha huyo wa mbio za masafa marefu alisema hapo awali alifika Uingereza kutoka Somalia na wazazi wake kama mkimbizi.

anasema wazazi wake hawajawahi kwenda Uingereza – mama yake na kaka zake wawili wanaishi kwenye shamba lao la familia katika jimbo lililojitenga la Somaliland.

Baba yake, Abdi, aliuawa kwa kupigwa risasi wakati Sir Mo alipokuwa na umri wa miaka minne, katika ghasia za kiraia nchini Somalia.

Somaliland ilijitangazia uhuru mwaka 1991 lakini haitambuliki kimataifa.

Sir Mo anasema alikuwa na umri wa miaka minane au tisa alipochukuliwa kutoka nyumbani na kukaa na familia yake nchini Djibouti.

Kisha alisafirishwa hadi Uingereza na mwanamke ambaye hajawahi kukutana naye na hakuwa na uhusiano naye.

Alimwambia kwamba alikuwa akipelekwa Ulaya kuishi na jamaa huko – jambo ambalo anasema “alifurahishwa” nalo.

“Sikuwahi kupanda ndege hapo awali,” anasema. Yule mwanamke akamwambia aseme anaitwa Mohamed. Anasema alikuwa na hati ghushi za kusafiria ambazo zilionesha picha yake karibu na jina “Mohamed Farah”.

Hati ghushi, inayoonyesha picha ya Sir Mo karibu na jina "Mohamed Farah", ilitumika kumpeleka nchini Uingereza.

Walipofika Uingereza, mwanamke huyo alimpeleka kwenye nyumba yake huko Hounslow, magharibi mwa London, na kuchukua kipande cha karatasi kutoka kwake ambacho kilikuwa na mawasiliano ya jamaa zake.

“Mbele yangu, alikichana na kukiweka kwenye pipa. Wakati huo, nilijua kuwa niko kwenye shida,” anasema.

Sir Mo anasema alilazimika kufanya kazi za nyumbani na malezi ya watoto ”nilipotaka kula chakula”.

Anasema mwanamke huyo alimwambia: “Ikiwa ungependa kuona familia yako tena, usiseme chochote.” “Mara nyingi nilijifungia bafuni na kulia,” anasema. Kwa miaka michache ya kwanza familia haikumruhusu kwenda shule, lakini alipokuwa na umri wa miaka 12 hivi alijiandikisha katika Mwaka wa 7 katika Chuo cha Jumuiya ya Feltham.

Wafanyakazi waliambiwa Sir Mo alikuwa mkimbizi kutoka Somalia.

Mkufunzi wake wa zamani Sarah Rennie anaiambia BBC kuwa alikuja shuleni “mnyonge na bila kujali”, kwamba alizungumza Kiingereza kidogo sana na alikuwa mtoto “aliyetengwa kihisia na kitamaduni”.

Anasema watu waliosema kuwa walikuwa wazazi wake hawakuhudhuria hafla zozote za jioni.

Mwalimu wa Sir Mo, Alan Watkinson, aliona mabadiliko kwa mvulana huyo alipokimbia mbio za riadha. “Lugha pekee ambayo alionekana kuelewa ni lugha ya PE na michezo,” anasema.

Sir Mo anasema michezo ilikuwa tegemeo kwake kwani “kitu pekee ambacho ningeweza kufanya ili kujiepusha na hali hii [ya maisha] ilikuwa ni kutoka na kukimbia”.

Hatimaye alimweleza Bw Watkinson kuhusu utambulisho wake wa kweli, historia yake, na familia aliyokuwa akilazimishwa kuifanyia kazi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents