Habari

Mollel ajinyakulia zaidi ya Milioni sita mashindano ya Lina PG Tour

Mkoa wa Arusha umeibuka kinara wa jumla wa raundi ya tatu ya mashindano ya gofu ya Lina PG Tour baada ya wawakilishi wake Nuru Mollel kushika nafasi ya kwanza na Elisante Lemeris kushika nafasi ya pili kwa wachezaji wa kulipwa.

Michuano hiyo iliandaliwa na familia ya Nkya na Chama cha cha Wanawake Tanzania (TLGU) ambapo ilishirikisha wachezaji wengi wa kulipwa na ridhaa kwa ajili ya kumuenzi Lina aliyefariki dunia Januari 19, 2021. Mchezaji huyo wa zamani alikuwa pia kiongozi wa TLGU.

Michuano hiyo ya mashimo 72 ilifanyka katika viwanja vya Gymkhana vya Arusha kuanzia Alhamisi, Julai 11 na kumalizika siku ya Jumapili, Julai 14 mwaka huu ambavyo ilishuhudia wacheza gofu wa Arusha wakichukua nafasi zote za juu kwa gofu ya kulipwa na ridhaa.

Wote, Nuru Mollel aliyeshinda kwa upande wa Mapro amejichukulia kiasi cha Sh. Milioni 6.8 na Elisante Lembris aliyemaliza wa pili amejipatia kiasi cha Sh. Milioni 4.3, wanatoka Arusha.

Mchezaji Jay Nathwani, Aliabass Kermali na Garv Chadhar walioshinda nafasi tatu za juu kwa gofu ya ridhaa, pia ni kutoka Arusha.

“Nimepambana sana hasa siku ya mwisho na kuweza kushinda kwa alama +8 mpaka mwisho. Lakini kazi hii ilikuwa ngumu mno alisema,” alisema Mollel na kuongeza

“Familia hii ya Nkya imefanya jambo kubwa sana, kwanza kutoa zawadi nzuri namna hii kwa washindi hii inafanya mchezo huu wa gofu kuwa wenye ushindani mkubwa zaidi na itawaleta wachezaji wengi zaidi, nina imani kubwa mashindano mengine yanayokuja wachezaji wengi zaidi watajitokeza,” alisema

Lembris ambaye aliongoza kwa siku tatu mfululizo, alimaliza katika nafasi ya pili kwa kupata alama +11 na nafasi ya tatu kushikwa na Isack Wanyeche aliyepata alama + 27 na kujinyakuliwa zawadi ya fedha kiasi cha Sh. Milioni 3.4.

Wengine walioshinda zawadi ya fedha taslim ni John Saidi mwenye alama 30 katika nafasi ya nne alipata kiasi cha Sh. Milioni 2.7 wakati nafasi ya tano ilishikwa na Frank Mwinuka mwenye alama +30 ambaye alipata Milioni 2 na wa sita akawa Fadhil Nkya mwenye alama + 32 aliyepata kiasi cha Sh. 480,000.

Kwa upande wa gofu ya ridhaa, Arusha iling’ara tena kwa kuchkua nafasi tatu za juu kupitia Jay Nathwani, Aliabass Kermali na Garv Chadhar

“Namshukuru Mungu kwa kunijalia kufanya vizuri kwani vita ya ushindi ilikuwa ngumu sana,” alisema Nathwani na kudai uzoefu wake wa uwanja umemsaidia pia.

Hii ilikuwa ni raundi ya tatu ya mfululizo wa Lina PG Tour baadqa ya zile mbili za awali kufanyika katika viwanja vya TPC Moshi na Morogoro.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents