Mradi wa JNHPP; hakikisho la upatikanaji wa umeme wa uhakika na nafuu Tanzania

Na Janeth Jovin, Dar es Salaam
Upatikanaji wa umeme wa uhakika na nafuu ni msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa taifa lolote.
Huku Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ikisukuma mbele miradi ya kimkakati, mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) unaojengwa kando ya Mto Rufiji unajitokeza kama kielelezo cha mafanikio makubwa katika sekta ya nishati.
Mradi huo, wenye thamani ya Shilingi trilioni 6.6, unatarajiwa kuzalisha megawati 2115 za umeme, hatua ambayo itaondoa tatizo la upungufu wa umeme nchini kwa kuhakikisha upatikanaji wa nishati hii hata katika vipindi vya ukosefu wa mvua.
Rais Samia aliongoza hafla ya kufunga njia ya kuchepusha maji na kuanza kujaza bwawa hilo mnamo Desemba 22, 2023, akisisitiza kuwa mradi huu utaongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme na kufungua fursa za kiuchumi na kijamii, ikiwemo ajira na utalii katika hifadhi za kusini mwa Tanzania.
“Itakumbukwa kuwa mradi huu ulianza kwa mkataba wa dola za Marekani bilioni 2.9 baina ya Tanzania na Misri mnamo Desemba 2018, ambapo ujenzi ulianza mwaka 2019. Huu ni mwanzo wa safari ya mageuzi ambayo inaunganisha mataifa na kuleta maendeleo kwa pamoja,” alisema Rais Samia.
Ufanisi na uwezo wa Mradi wa JNHPP
Dk. Khatibu Kazungu, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia masuala ya umeme na nishati jadidifu, alisema kuwa mradi wa JNHPP tayari una uwezo wa kuzalisha megawati 700, na unatarajiwa kufikia megawati 900 hivi karibuni.
“Hii ni hatua muhimu inayoweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuwa na nishati ya kutosha na hata kuuza nje ya nchi,” alieleza Kazungu wakati wa mahojiano na Bongo 5.
Kazungu alibainisha kuwa vyanzo vingine vya nishati vinavyohimizwa ni pamoja na umeme wa jua, unaoweza kuzalisha megawati 600, na jotoardhi lenye uwezo wa kuzalisha megawati 5000. Hii inaonesha kuwa Tanzania ina hazina kubwa ya nishati ambayo inaweza kuendelezwa ili kukidhi mahitaji ya umeme ya taifa.
Mradi wa gridi imara
Kazungu aliongeza kuwa Serikali inaendelea na mradi wa Gridi Imara ambao unalenga kuboresha miundombinu ya umeme na kuendeleza vyanzo vipya ili kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana kote nchini.
“Ni lazima tujipange vizuri kama serikali kujua jinsi ya kuongeza megawati kupitia vyanzo hivi vingine ili kutimiza mahitaji ya umeme nchini,” alisema Kazungu.
Maendeleo ya Mradi wa JNHPP na muda wa kukamilika
Akihutubia Bungeni kuhusu bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2024/2025, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, alisema kuwa mradi wa JNHPP unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2024 miezi miwili ijayo, ambapo mitambo yote tisa, yenye uwezo wa kuzalisha megawati 235 kila moja, itakuwa inafanya kazi.
Anafafanua kuwa kwa sasa, mtambo wa kwanza unazalisha megawati 235, na mradi upo kwenye hatua ya mwisho ya ujenzi, ukiwa umekamilika kwa asilimia 98.01.

Wananchi watoa maoni yao kuhusu faida za Mradi wa JNHPP
Wananchi mbalimbali wameelezea matumaini yao kuhusu faida za mradi huo kwa uchumi wa taifa. Anna Kalokola, mkazi wa Kifuru, alisema, “Tunashukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia kwa kutekeleza mradi huu. Uhakika wa umeme utaboresha huduma za kijamii na kuvutia uwekezaji, hasa kwenye sekta ya viwanda.”
Silayo Moses, mkazi wa Ubungo Dar es Salaam, alisema kuwa mradi huu ni hatua kubwa kwa Tanzania. Huku akionyesha matumaini ya Tanzania kuuza umeme nje ya nchi, Moses alisema,
“Ikiwa tunataka kuuza umeme nje, ni muhimu kutumia vyanzo vyote vya nishati vilivyopo kama jua na jotoardhi ili tujihakikishie nishati ya kutosha,” alisema.
Kwa upande wake Hilda Raphael mkazi wa Mbagala alisema Serikali inayoongozwa na Rais Samia imeamua kwa dhati kuwekeza katika miradi ya nishati nchini lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa upatikanaji umeme nchini unakuwa mkubwa kuliko mahitaji ya nchi.
Alisema yeye ni mama wa nyumbani lakini amekuwa akitengeneza juisi hivyo utegemea umeme wakati akifanya shughuli hiyo inayomuingizia kipato cha kuendesha familia yake.
“Nimeona na kusikia mradi huu wa bwawa la Nyerere ukikamilika tutakuwa na uhakika wa umeme nami natamani tusiwe na mgao wala kukatika kwa umeme, hii itasaidia sana kwa wafanyabiashara wanaotegemea umeme kuwa na uhakika wa biashara zao.
“Niiombe serikali ihakikishe mradi huu unakamilika kwa wakati uliyopangwa ili wananchi wanufaike na uwepo wa mradi,” alisema Hilda

Aidha alisema anaimani na serikali ya Rais Samia kwani itatekeleza na miradi mingine ya maendeleo inaotekelezwa ikiwemo ya miundombinu ya Barabara ili kuondoa changamoto za foleni katikati ya jiji la Dar es Salaam.
“Tukiwa tunauangalia mradi huu tusisahau kuwa kuna utekelezaji wa miundombinu ya Barabara unaoendelea sasa tunaomba ujenzi huu ukamilike kwa wakati maana kwa sasa huko barabarani foleni ni kubwa, ni Imani yangu mambo haya yakikamilika kila mwananchi atafurahi” alisema
Mradi wa JNHPP unaonesha dhamira ya Tanzania katika kufikia lengo la kuwa na umeme wa uhakika kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Huku ukitegemewa kuboresha maisha ya Watanzania wengi na kuongeza mapato kupitia mauzo ya umeme nje, mradi huu ni kielelezo cha sera thabiti za Serikali ya Rais Samia katika kuboresha sekta ya nishati.
Written by Janeth Jovin