Michezo

Mshambuliaji hatari Afrika asaini Simba

SIMBA wako siriazi na mambo yanakwenda kimyakimya. Arena tunajua mpaka jana jioni kwa uchache ilishamalizana na majembe mawili. Lameck Lawi (Coastal Union) huyu ni beki. Serge Pokou (Asec) ni kiungo. Lakini hata Yusuph Kagoma (Singida FG) kila kitu kimeshakamilika kwa asilimia kubwa. Ishu ya kocha wako kwenye hatua za mwisho kumalizana na Steve Komphela kutoka Afrika Kusini.

Sasa imefikia pazuri kumsainisha mkataba wa miaka miwili straika wa Uganda  Steven Mukwala (24) anakiwasha kwenye klabu ya Asante Kotoko ya Ghana. Wekundu wa Msimbazi hao wamepania kurejesha ufalme wao uliofifia kwa misimu mitatu nyuma ambapo wameamua kuvunja benki ili kushusha wachezaji wa maana.

Mukwala leo Ijumaa atakuwa kwenye Uwanja wa Mandela nchini Uganda akiiongoza timu yake ya taifa, kuivaa Botswana katika mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia. Mukwala ni mfungaji bora namba mbili katika msimu uliomalizika wa ligi ya Ghana akifunga mabao 14 nyuma ya kinara Stephen Amankonah wa Berekum Chelsea aliyecheka na nyavu mara 16.

Mukwala anasifika kwa kasi, mashuti na umahiri wa kufunga amemaliza mkataba na Kotoko lakini wakali hao wa Ghana wameonyesha nia ya kumuongezea mkataba mpya ila Mukwala amegoma kusaini huku akiwaeleza anaondoka kwenda kutafuta changamoto mpya. Arena tumegundua Simba ndiyo imempa kiburi Mukwala kutoongeza mkataba mpya kwa kumuahidi kumsaini na kumpa bonasi kubwa jambo lililomvutia haswa akiangalia hamasa iliyopo kwenye ligi hiyo kwasasa. .

Arena tunajua Simba imewasiliana na Mukwala na pande hizo mbili zimekubaliana kukutana baada ya mechi za timu za taifa kwa mazungumzo ya mwisho ya dili hilo. “Kama kila kitu kitaenda tulivyopanga basi atasaini mkataba wa miaka miwili,” alidokeza mmoja ya viongozi wa juu wa Simba ambayo imeunda kamati mpya ya usajili yenye sura zenye uzoefu kama Cresentius Magori, Mulamu Nghambi na Kassim Dewji.

 

 

 

 

 

 

 

 

Imeandikwa na Mbanga B.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents