Msigwa awaita CAF wakague tena kwa Mkapa

Baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kutoa tangazo la kuufungia Uwanja wa Michezo wa Benjamin Mkapa, Serikali imesema walitakiwa kuwasiliana nao kabla ya kuufungia kwa sababu ulishakarabatiwa.
Akizungumza leo Machi 12,2025, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,Gerson Msigwa amethibitisha kupokelewa kwa tangazo la kuufungia uwanja huo leo asubuhi.
“Ni kweli leo wameamka na hiyo taarifa kuwa CAF wameufunga uwanja wa Benjamin Mkapa kwa sababu za dosari katika eneo la kuchezea. Ukaguzi wa CAF ulifanyika kama wiki mbili zilizopita na ulifanyika baada ya mechi ya Simba na Azam na kumbukeni sisi uwanja tulishautangaza kuufunga kupisha ukarabati,”amesema.
“Lakini hizi mechi zinakuwa na mashabiki wengi na mambo mengi ya kiusalama. TFF (Shirikisho la mpira wa Miguu Tanzania) likatuomba tunaomba tutumie uwanja, siku wamekuja pale uwanja ulikuwa umekatwa nyasi hadi chini kabisa. Kwa hiyo wachezaji walipokuwa wanacheza na unajua hizi mechi zina presha kidogo ukaenda unachimbika chimbika kidogo,”amesema.
Msigwa ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, amesema wakati wanacheza mchezo huo, wakaguzi wa CAF walikuwepo na waliwaeleza kuwa wahakikishe wanarekebisha na wakataka kuona mashine za kurekebishia sehemu ya kuchezea (pitch).
cc; Mwananchi