Habari

Msigwa: Tanzania bado inahitaji wawekezaji wengi wakiwemo kutoka Urusi

TANZANIA bado inahitaji wawekezaji wengi zaidi katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, madini, utalii, michezo na sanaa na kwamba nchi inawakaribisha wawekezaji kutoa Urusi kuwekeza katika sekta hizo.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa wakati wa siku maalum ya Urusi iliyofanyika katika viwanja vya Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara maarufu sabasaba.

Msigwa ametoa wito kwa sekta binafsi ya Urusi kuja Tanzania kuchangamkia fursa nyingi ambazo bado hazijatumika na kwamba serikali imeweka utaratibu mzuri ambao kila mfanyabiashara na wawekezaji kutoka nchi mbalimbali wataweza kupata kwa haraka vibali vya uwekezaji.

“Tumeweka pia vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi ambavyo vitawawezesha wawekezaji kuwekeza kwa faida hapa nchini, wawekezaji wakija kuwekeza nchini watakuwa na uwezo kunufaika na soko la kibiashara lenye watu zaidi ya Milioni 177 kwa Afrika Mashariki,” amesema Msigwa na kuongeza

“Nchi inapohimiza wawekezaji kuja kuwekeza hapa nchini, watanzania wanapata fursa ya kuona fursa zilizopo kwenye nchi za wawekezaji hao, moja ya fursa ya kushirikiana nao tunanufaika na mengi kwa kupata ujuzi ambao unatusaidia kuboresha uzalishaji na njia zetu za kibiashara,” amesema

Amesisitiza kwa sasa Tanzania bado inahitaji uwekezaji mkubwa, na kuongeza kuwa uwiano wa kibiashara kati ya Urusi na Tanzania haupo sawa.

“Sisi tunauza Urusi bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 6.4 ila wenzetu Urusi wanauza Tanzania bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 179, hii ni fedha nyingi maana yake wao wanapata zaidi ila sisi tunapata kidogo hivyo kupitia mikutano kama hii pamoja na ile ya sekta binafsi ya Tanzania na Urusi wanajadiliana juu ya mbinu mbalimbali zinazoweza kutumika kuimarisha ufanyaji wa biashara pande zote mbili,” amesema

Kwa upande wake Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Andrey Avetisyan amesema Urusii po tayari kuwekeza Tanzania na kwamba makongamano ni muhimu kwa wafanyabiashara wan chi zote mbili.

Amesema kupitia kongamano hilo maalum wafanyabiashara kutoka Urusi na Tanzania wanaweza kubadilishana uzoefu na kupeana fursa za uwekezaji.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents