
“Kuna vitu vingi tunaviangalia kabla mchezaji hajaenda kwenye timu, Mzize ndio kwanza ana miaka 21! Hatutaki kumbilia fedha zaidi badala yake tunaangalia sana kesho yake itakuwa bora akiwa wapi.
Timu ambayo inammiliki [Yanga] na yenyewe ina matakwa yake, wanaweza kusema wanahitaji kiasi fulani ili wamuuze kwa sababu wamewekeza kiasi fulani kwake. Hivyo ni miongoni mwa vitu tunavyojadili na ninaamini mwafaka utapatikana kwa sababu Mzize ni kijana ambaye ameiheshimu Yanga kwa hiyo hawawezi kumzuia kuondoka.
Kumzuia Mzize kuondoka ni kumnyima kuendelea na kumnyima kupata maslahi zaidi ambayo hata wenyewe wanajua hataweza kuyafikia kutokana na mshahara ambao ameahidiwa huko nje.
Wydad Casablanca inamuhitaji sana Mzize na haijaanza sasa hivi bali ni muda mrefu kwa sababu Kocha Mokwena tangu ameingia pale amekuwa akihitaji mshambuliaji na chaguo lake la kwanza ni Mzize.
Mokwena ni shabiki sana wa Mzize, mimi nazungumza nae na ananiambia anamtaka Mzize awe nae hata kama sio Wydad basi kwenye timu nyingine atakayokuwepo. Kwa hiyo ni kweli wanamuhitaji na waliongea na Rais wa Yanga [Eng. Hersi Said] akawajibu kuwa anataka Mzize abaki Yanga hadi atakapomaliza msimu.
Kwa hiyo tunaheshimu alichokisema Rais wa Yanga na Mzize mwenyewe karidhia hataki kuondoka kwa fujo. Akimaliza msimu tutakaa mezani na kuangalia kama itakuwa Wydad, England, Saud Arabia au Afrika Kusini. Tutajadili ofa zote itakayokuwa na maslahi kwa mchezaji basi Yanga itamruhusu mchezaji aende mbele.
— JASMINE RAZACK, MSIMAMIZI WA MZIZE.