MUCE yabuni dawa ya kumuua mdudu ‘kantangaze’ anayeharibu nyanya shambani

WAKULIMA wa nyanya nchini wanaopoteza jasho lao shambani kutokana na kusumbuliwa na wadudu waharibifu wa mazao waitwao ‘Kantangaze’, sasa wamepata ahueni baada ya watafiti kugundua namna mpya ya kuwaangamiza.
Idara ya Kemia ya Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) kilichopo Manispaa ya Iringa, kimefanya utafiti na kuja na dawa hiyo ya kumdhibiti mdudu huyo .
Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea Viwanja vya sabasaba jijini Dar es Salaam, Juma Mmongoyo kutoka idara hiyo anasema yeye pamoja na wenzake ambao ni Asha Kiunga, Frank Dickson, Selemani Juma, Agenor Mafra Neto, Fikira Kimbokota, Dk. Chaymae Fennine pamoja na Profesa Teun Dekker Ndio kwa pamoja waliofanya utafiti na kubuni dawa hiyo.
Amesema waliamua kufanya utafiti na kuja na dawa hiyo baada ya kuona wakulima wa nyanya hawana furaha kwa sababu ya mdudu huyo mharibifu ambaye anawafanya watumie dawa nyingi za gharama kuhudumia mashamba yao ili waweze kupata mavuno.
Mmongoyo amesema wameamua kuuleta sabasaba mradi wao huo wa kupambana na mdudu huyo mharibifu ili wakulima wa nyanya waweze kuuona namna unavyofanya kazi.
“Bado tunaendelea na utafiti wa dawa hii hata hivyo matokeo yake yameanza kutupa moyo kwa sababu dawa inafanya vizuri kwa kuondosha mazaria ya mayai ya mdudu katika mashamba na hivyo wakulima katika shamba la mradi hawatumii tena dawa ,” amesema
Dawa inavyofanyakazi
Mmongoyo amesema dawa hiyo inauwezo wa kumvuta madume ya mdudu kantangaze badala ya kupata majike yao ambayo yanauwezo wa kutoa kemikali kwa ajili ya kumpatia taarifa ya uwepo wake ili aweze kuzalisha mayai.
“Taarifa zilizopo mdudu mmoja wa kike anauwezo wa kuzalisha mayai 3000, hivyo tukiwaacha waendelee wanaharibu nyanya, sisi tunachofanya katika utafiti wetu tuna hakikiisha madume ya kantangaze hayapati nafasi ya kukutana na majike ya kantangaze kwa kuwapa harufu inayofanana na majike hayo.
“Harufu hiyo inawadanganya madume wakidhani kuwa wanakwenda kwenye majike ya kantangaze kumbe wa kwenda kwenye dawa na wanauawa hivyo tunaondosha uwezekano wa kuzalisha hayo mayai,” amesema
Aidha amesema faida ya mradi huo utampunguzia mkulima gharama za kununua dawa kwa ajili ya kuua wadudu hao katika mashamba yao.
Written by Janeth Jovin