Muhimbili yamuaga Dk. Rwegasha anayekwenda AU

Menejimenti ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo kwa niaba ya wafanyakazi wote imemuaga rasmi Dkt. John Rwegasha, aliyekuwa Mkurugezi wa Huduma za Tiba hospitalini hapo baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Tiba katika Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) ambapo anatarajiwa kuanza majukumu yake mapya Februari 2025 huko Addis Ababa, Ethiopia.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi, ameeleza mchango mkubwa wa Dkt. Rwegasha alioutoa na kuleta ufanisi mkubwa katika kuboresha huduma za afya hospitalini hapo na kumtakia kila la kheri na uwakilishi mzuri wa Tanzania katika kutekeleza majukumu yake nchini humo.
“Dkt. Rwegasha amekuwa mfano wa kiongozi anayefanya kazi kwa ufanisi na kujituma tunampongeza kwa juhudi zake, tunamtakia kila la kheri katika nafasi yake mpya, tunaamini ataiwakilisha vyema Tanzania katika utendaji wake ndani ya AU,” amesisitiza Prof. Janabi.
Kwa upande wake, Dkt. Rwegasha ameushukuru Uongozi wa MNH na wafanyakazi wenzake kwa ushirikiano mkubwa alioupata katika kutekeleza majukumu yake kama Mkurugenzi wa Huduma za Tiba hospitalini hapo na kuahidi kuiwakilisha vema Tanzania katika nafasi hiyo.
Written by Janeth Jovin