Picha

Muuguzi amchoma binti sindano ya usingizi na kisha kumbaka, Yaelezwa msichana alikuwa hospitalini akimuuguza mama yake

Imeelezwa kuwa muuguzi  mmoja wa Hospitali ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Anatuhumiwa kumbaka msichana wa miaka 16 (Jina linahifadhiwa), mkazi wa Mtaa wa Buyumba, Kata ya Igunga Mjini.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Mganga Mkuu Wilaya ya Igunga, Dkt. Ruta Deus amesema binti huyo alikuwa akimuuguza mama yake aliyekuwa amelazwa hospitalini hapo.

Ni kweli tukio hilo lipo na hiyo si mara ya kwanza kwani siku za nyuma muuguzi huyo (jina tunalo) akiwa Kituo cha Afya Tarafa ya Igurubi alifanya tukio kama hilo, hivyo hii ni mara ya pilli na huo ni ukiukwaji wa taratibu na kanuni za kiutumishi,” alisema Dkt. Deus.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini hapo, Mamamzazi wa msichana huyo, Wande Salum (42) aliyekuwa amelazwa wodi no. 3, alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 10, mwaka huu, saa 4 usiku.

Wande alidai kuwa muuguzi huyo alifika katika wodi hiyo kuangalia hali yake na baada ya kumuona alimwambia ambadilishe dawa na alimuomba aondoke na mwanae aliyekuwa akimuuguza na walipofika ofisini alimchoma sindano ya usingizi kisha kumbaka kuanzia saa 4 usiku hadi saa 8.

Bi. Wande amesema baada ya kuona muda unaenda pasipo mwanawe kurudi wodini, Aliomba msaada kwa baadhi ya wagonjwa wenzake wenye hali nzuri wamsaidie kumtafuta.

Alidai kuwa baadhi ya manesi waliokuwa zamu walipopata taarifa hiyo, waliungana na baadhi ya wagonjwa kumtafuta mwanawe na walimkuta eneo la nyasi wanakofulia nguo kina mama akiwa hajitambui, huku akivuja damu sehemu za siri kutokana na kubakwa kwa muda mrefu na muuguzi huyo.

Aidha mama huyo alisema kitendo alichofanyiwa mwanawe ni cha kinyama na hakipaswi kufumbiwa macho, huku akiomba vyombo vya dola kumsaka muuguzi huyo apatikane na kufikishwa mahakamani.

Baadhi ya kina mama wanaokwenda kutibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga, Rehema Julias na Sada Mwinamila, walisema hivi sasa wameingiwa na hofu kutokana na kitendo hicho na kuiomba Serikali kutofumbia macho suala hilo.

Mganga Mkuu amesema kuwa tayari suala hilo liko polisi na wao wanaendelea kuchukua hatua dhidi ya muuguzi huyo ambaye mpaka sasa hapatikani kwa njia ya simu na hajulikani yupo wapi.

Mkuu wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Barnabas Mwakalukwa, Walipoulizwa kuhusu tuhuma hizo dhidi ya muuguzi huyo, walisema bado hawajapokea taarifa hizo.

CHANZO: Mtanzania

Related Articles

Back to top button