Habari

Muungano wa upinzani, NASA wasambaratika

Upinzani nchini Kenya unafungua ukurasa mpya baada ya chama cha Orange Democratic Movement ODM kujiondoa kwenye muungano wa NASA muda mfupi baada ya vyama tanzu vya WIPER na ANC kujitenga nao.

Siasa za nchini Kenya kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 zinazidi kushika kasi. Muungano wa NASA unasambaratika, huku muungano mpya wa Okoa Kenya Alliance ukikabiliwa na misukosuko kwa kuwa wadau watarajiwa bado hawajafikiana kuhusu mustakabali wao. Chama tawala cha Jubilee nacho kiko kwenye harakati za kumnadi kiongozi wa ODM Raila Odinga katika eneo la Mlima Kenya.

Muda mfupi uliopita chama cha Orange Democratic Movement, ODM kilitangaza kujiondoa rasmi kwenye muungano wa upinzani wa NASA ambao umekuwa ukilegalega. Tofauti zilijiri baada ya mzozo wa kugawa ruzuku ya vyama vya kisiasa kuzuka. Kwa sasa ODM inatishia kutowagawia wadau wa NASA ruzuku hiyo ya jumla ya shilingi milioni 153. Kwenye kikao cha baraza kuu la ODM, wanachama wanawarai wadau kubadili mitazamo yao.

Muungano mpya wa Okoa Kenya, OKA, ambao haujarasimishwa unawaleta pamoja viongozi wa KANU, Gideon Moi, Kalonzo Musyoka wa Wiper, Moses Wetangula wa Ford -Kenya na Musalia Mudavadi wa ANC.Duru zinaashiria kuwa kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi anang’ang’ania kuwa mpeperusha bendera ya muungano wa Okoa Kenya jambo ambalo linazua mitazamo tofauti.

Wakati hayo yakiendelea washirika wa karibu wa Rais Uhuru Kenyatta wanaotokea eneo la Mlima Kenya wanafanya kikao hii leo kuandaa mikakati ya kumnadi kiongozi wa Orange Democratic Movement,ODM Raila Odinga kwa wakaazi wa eneo la kati.Hii ni mara ya kwanza kwa wanasiasa wa eneo hilo kuja pamoja kumpa ridhaa Raila Odinga kuwa mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta.Mpango huo una azma ya kukabiliana na naibu wa Rais William Ruto anayeendelea kunadi sera zake kwenye eneo hilo la Mlima Kenya anakotokea Rais Uhuru Kenyatta.

By-BAKARI WAZIRI

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents