Mwanajeshi akatwa kwa kuwa Jasusi
Mwanajeshi wa zamani wa jeshi la Uingereza Daniel Khalife amepatikana na hatia ya kufanya ujasusi kwa ajili ya Iran.
Khalife, ambaye alitoroka jela wakati akisubiri kesi yake, alikusanya taarifa na kuzifikisha Tehran na imebainika kuwa amekusanya majina ya askari wa kikosi maalumu.
Aliondolewa shtaka la kutekeleza udanganyifu wa bomu la uongo kwenye kambi yake ya jeshi.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 23 alikiri kutoroka gereza la Wandsworth huko London mwezi Septemba 2023, kwa kujifucha chini ya lori la kupeleka chakula wakati wa kesi yake katika Mahakama ya Woolwich.
Jaji Bobbie Cheema-Grubb amesema katika Mahakama ya Woolwich Corwn kwamba Khalife anaweza kukabiliwa na “hukumu ya kifungo cha muda mrefu” atakapohukumiwa mapema mwaka ujao.
Vitendo vyake vilikiuka sheria kuhusu siri na sheria ya Ugaidi na hakuonesha kujuta wakati akipatikana na hatia.
Waendesha mashtaka wanasema Khalife aliwasiliana na mtu anayehusishwa na ujasusi wa Iran mara tu baada ya kujiunga na jeshi Septemba 2018, kabla ya kuwaambia MI6 kuwa alitaka kuwa jasusi wa nchi mbili.
Mahakama ilielezwa kuwa, alikusanya taarifa nyeti na kuzipeleka kwa watu wasiofaa na hilo lilileta hatari kubwa katika mikono isiyofaa.
Khalife aliwasiliana na mwanaume anayehusishwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) kwenye Facebook.
Alijenga uhusiano na maafisa wa Iran – na wakati mmoja alitumiwa dola za Kimarekani 2,000 – na kutakiwa kuzichua katika mfuko katika bustani ya London kaskazini.
Wakati akihudumu jeshini, Khalife alikusanya majina ya wanajeshi 15 – wakiwemo baadhi kutoka katika kikosi maalumu.
Waendesha mashtaka wanaamini alituma orodha hiyo kwenda Iran kabla ya kufuta ushahidi wowote.
Alikanusha kutuma taarifa hizo na kudai kuwa taarifa alizotoa zilikuwa za uwongo. Lakini, inaonekana alituma hati mbili – moja kwenye kuhusu ndege zisizo na rubani na nyingine kuhusu “habari za kijasusi, Ufuatiliaji na taarifa za kijeshi.”
Uingereza kujua taarifa nyingine nyeti ambazo Khalife alizipeleka – kwani jumbe nyingi alizotumia na waasiliani kwenye programu ya mawasiliano ya njia fiche ya Telegram zilifutwa.
Khalife alisakwa baada ya kutoroka gerezani , kabla ya kukamatwa saa 75 baadaye alipoonekana akiendesha baiskeli karibu na mto. Alifanya jaribio la kuwasiliana na Wairani kabla ya kupatikana, na kutuma ujumbe wa Telegram ambao ulisema: “Nasubiri.”
Kutoroka kwa Khalife kutoka gereza la Wandsworth kulizua maswali mazito kuhusu usalama na wafanyakazi katika gereza hilo, na kupelekea wafungwa 40 kuhamishwa kwa muda kupisha uchunguzi wa tukio hilo ukifanyika .