Michezo

Mwanariadha wa Kenya aondolewa Olimpiki kisa matumizi ya madawa

Mwanariadha wa Kenya Mark Otieno Odhiambo ameondoshwa nje ya mashindano ya Olimpiki ya Tokyo baada ya vipimo kuonesha ametumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni.

Kijana huyo wa miaka 28 alikuwa ametakiwa kushindana katika mbio za mita 100 za wanaume Jumamosi lakini alishindwa katika hatua ya vipimo na kubainika alitumia dawa za kusisimua misuli.

Kwa mujibu wa mkuu wa msafara huko Tokyo Waithaka Kioni: “Hata hivyo amekataa kutambua madai ya ukiukaji huo na kuomba uchambuzi wa sampuli yake ya mkojo .”

Kipimo kilifanyika tarehe 28 mwezi Julai wakati mwanariadha huyo alipokuwa Tokyo, kabla ya hapo alikuwa kwenye kambi ya mazoezi nchini Japan kati ya tarehe 15 na tarehe 24 mwezi Julai.

Otieno Odhiambo alishiriki kwenye Mashindano ya Dunia ya 2017 na Michezo ya Jumuiya ya Madola ya 2018.

Ni mwanariadha wa pili wa Kiafrika kuondolewa kwenye michuano hiyo baada ya Mnaijeria Blessing Okagbare.

Kioni alisisitiza kwamba maafisa wa michezo na bodi zinazosimamia michezo nchini Kenya wameazimia kuendeleza vita yao dhidi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni

”Haya ni mambo ambayo labda yanaweza kuepukika hii ndio sababu inaendelea kuwasiliana na mashirikisho ya michezo na ADAK kwa hivyo tunaendelea kutoa elimu juu ya kupambana na dawa zilizopigwa marufuku kwa wanariadha wetu, “aliiambia BBC Sport Africa.

“Lakini sio kwamba wanariadha hawajui na ndio sababu tunachukulia kuwa hana hatia hadi tutakapochunguza tena sampuli B ya mkojo.

“Nilizungumza naye mchana huu na ananiambia hawezi kukumbuka kama alitumia kitu chochote ambacho kitatoa matokeo ya aina hiyo.

“Kinachonisumbua ni kwamba Kenya tayari imekuwa kwenye orodha ya waliowekewa alama nyekundu na tulitarajia tutatoka katika orodha hiyo lakini tukio kama hili linaweza kuvuruga mpango wa kujinasua.”

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents