Mwenge wa Uhuru waweka jiwe la msingi kiwanda cha kusaga kokoto cha Bilioni 3 Songea

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda ameweka jiwe la msingi la mradi wa kiwanda cha kusaga kokoto cha Kampuni ya OVANSI kilichopo Kijiji cha Lipokela, Kata ya Mbinga Mhalule, Halmashauri ya Wilaya ya Songea, huku akieleza kuridhishwa kwake na utekelezaji wa mradi huo wenye lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo.
Amepongeza uwekezaji huo akisema unaonesha namna sekta binafsi inavyoendelea kushiriki katika kuimarisha uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.
Mradi huo unaogharimu shilingi bilioni 3 unatajwa kuwa miongoni mwa uwekezaji mkubwa wa kimkakati katika Wilaya ya Songea, ukilenga kuongeza upatikanaji wa kokoto kwa matumizi mbalimbali ya ujenzi pamoja na kutoa ajira kwa wananchi zaidi ya 100.
Kiwanda hicho kinatarajiwa kusaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa malighafi za ujenzi na kuongeza kasi ya maendeleo ya miundombinu katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Ruvuma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwang’onda ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji nchini, hali inayochochea ukuaji wa sekta binafsi na maendeleo ya wananchi.
Amesema amani na mshikamano uliopo nchini ni msingi muhimu wa maendeleo na uwekezaji endelevu, huku akiipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Songea kwa ushirikiano wake katika kufanikisha mradi huo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Dkt. Bunungu amesema mashine za kisasa zilizowekwa katika kiwanda hicho zina uwezo wa kuchambua aina tisa za kokoto, jambo litakaloongeza ufanisi wa uzalishaji na kukidhi mahitaji ya soko.
Ameongeza kuwa uwekezaji huo utafungua fursa zaidi za ajira, kuinua kipato cha wananchi na kuwa kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo la Songea na maeneo ya jirani.
Written by Angel Kayombo






