Mzize awakataa Waarabu, Ulaya freshi

DILI kibao zimetua mezani kwa mabosi wa Yanga kutoka timu zinazotaka kumsajili mshambuliaji Clement Mzize (20) zikiwamo kutoka Afrika Kaskazini, Saudia Arabia na Ulaya, lakini straika huyo mwenye mabao 13 kwa sasa Ligi Kuu Bara amezichomolea za Kiarabu, huku ikielezwa hesabu zake ni kutaka kucheza Ulaya.
.
Ofa ya awali ambayo Yanga iliichomoa ilikuwa ni ya Wydad Casablanca ya Morocco na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, kabla ya klabu moja ya Saudi Arabia na nyingine ya barani Ulaya zinazomtaka Mzize. Hivi karibuni ikaelezwa kuwa klabu mbili za Ufaransa za Olympique Lyonnais na AS Saint-Etienne zinazoshiriki Ligue 1 zinadaiwa zimeonyesha nia ya kumtaka mchezaji huyo mbali na klabu moja ya Ubelgiji na kuwafanya mabosi wa Jangwani kukuna vichwa wakipima uzito wa mzigo watakaopewa.
.
Hata hivyo, inaelezwa Mzize amewaambia mabosi wanaomsimamia kwamba anataka kwenda kucheza Ulaya na ishu za timu za Uarabuni hana mpango nazo. Inaelezwa kwamba ofa zilizowekwa na timu za Ulaya ni kubwa na zilizomvutia mchezaji huyo tofauti na klabu za Afrika Kaskazini au Saudia Arabia.