Habari

Naibu Waziri atoa siku 10 mizani ya Nyakahura, Kagera kukamilika

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ametoa siku 10 kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Kagera, kuhakikisha anamsimamia mkandarasi anayejenga mizani ya Nyakahura mkoani humo,  kumaliza ujenzi na kuanza  kutolewa huduma za upimaji wa magari katika mizani hiyo kama zamani.

Akizungumza katika ziara yake ya kukagua miradi ya barabara, mizani na madaraja mkoani humo, Naibu Waziri Kasekenya, amesema kuwa kusimama kwa huduma za upimaji wa magari katika mizani hiyo kunaisabibishia Serikali hasara kubwa, kwani kupitia fursa hiyo magari yanaweza kuzidisha uzito na kupelekea kuharibu barabara.

“Ujenzi wa mizani hii inabidi ukamilike mapema iwezekanavyo, nimeambiwa hapa kwa siku yanaweza kupita magari zaidi ya 500, hivyo magari kutokupima hapa inaweza ikawa sababu ya wasafirishaji kuzidisha uzito na kupelekea kuharibu barabara zetu ambapo Serikali inatumia kiasi kikubwa cha fedha ili kuzijenga”, amesema Kasekenya.

Aidha, amemuagiza Meneja huyo kufanya utaratibu wa kuandaa mchoro wa mizani nyingine ya pili, pembezoni mwa mizani ya kwanza ili kuepusha msongamano amabao unaweza kujitokeza.

“Haiwezekani sehemu inayopitisha magari mengi kama hii ikawa na mizani moja ya kupima magari yanayotoka na yanayoingia nchini, hivyo nakuagiza tena Meneja kuandaa mchoro na kuuwasilisha Wizarani ili tutenge fedha kwa ajili ya mizani ya pili”, amesisitiza Kasekenya.

Kuhusu suala la barabara katika mkoa huo, Kasekenya amesema kuwa Serikali imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 12.8 kwa ajili ya ukarabati mdogo  wa barabara ya Lusahunga – Rusumo (Km 92), huku ikisubiri taratibu za manunuzi ya kumpata mkandarasi wa kufanya ukarabati mkubwa.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kasekenya, amekagua daraja la Kitengule lenye urefu wa mita 140 na barabara za maingilio zenye urefu wa kilometa 18 ambapo ameridhishwa na kasi ya ujenzi ya mradi huo unaojengwa na mkandarasi M/s China Henan.

Amebainisha kuwa daraja hilo ambalo linaunganisha wilaya ya Karagwe na Misenyi, litakuwa ni njia ya mkato kati ya wilaya hizo mbili na hivyo kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa wilaya hizo na mwekezaji wa kiwanda cha sukari kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la Ngara, Mheshimiwa Ndaisaba Ruhoro, ameipongeza Serikali kwa kutoa shilingi Bilioni 6  kwa ajili ya maandalizi ya kuanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami za Nyakahura – Kumubuga – Murusugamba (Km 75), Kumubuga – Rulenge – Mururama (Km 32) na Rulenge – Kabanga Nickel (Km 34) ambapo amesema kuwa kukamilika kwa barabara hizo kutarahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kutoka wilaya hiyo kuelekea wilaya jirani na hata nchi jirani za Rwanda na Burundi.

Naye, Msimamizi wa Daraja la Kitengule, Charles Rumisha, amesema kuwa mradi ulianza mwezi Oktoba, 2018 na kutarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu ambapo amesisitiza kuwa mpaka sasa wamefika katika hatua nzuri.

Amefafanua kuwa kwenye upande wa barabara ujenzi umefika asilimia 88 na kwa upande wa daraja mkandarasi tayari keshakamilisha ujenzi wa nguzo zote nne, kilichobaki ni kuweka usawa wa juu wa barabara.

Naibu Waziri Kasekenya, yupo katika ziara ya siku Tatu mkoani Kagera ambapo atakagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na na Wizara hiyo ili kujionea maendeleo yake.

                   Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents