Habari

NBC watoa gawio la Tsh Bil 20

Dar es Salaam, MEI 17, 2023 – Serikali imepokea kiasi cha TZS 6 bilioni kutoka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ikiwa ni sehemu ya gawio la kiasi cha Tsh bilioni 20 ambayo benki hiyo imetenga kwa ajili ya wanahisa wake kufuatia faida iliyopata katika kipindi cha mwaka 2022. Serikali inamiliki asilimia 30 ya hisa za benki hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi alikabidhi gawio hilo kwa Msajili wa Hazina Bw Nehemiah Mchechu aliewakilisha serikali wakati hafla fupi ya makabidhiano hayo iliyofanyika mapema leo jijini Dar es Salaam ikihudhuliwa na wadau mbalimbali kutoka serikali na maofisa waandamizi wa benki hiyo.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Bw Mchechu pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika kipindi cha mwaka 2022, aliwasilisha salamu za Rais Samia Suluhu ambae pia aliipongeza benki hiyo huku akitoa wito kwa taasisi na mashirika yenye umiliki wa umma kuhakikisha yanatimiza wajibu wao wa kuwasilisha gawio litokano na faida za uendeshaji wa shughuli zao kwa serikali.

“Serikali inafurahishwa na utendaji ulioimarika wa Benki ya NBC. Sisi kama wanahisa, tunafurahi kuona uwekezaji wetu unatoa matunda. Gawio la TZS6 bilioni ambalo Serikali ilipokea leo litaongeza ukubwa wa kapu letu la makusanyo ambayo yamekuwa yakielekezwa katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo hususani ile ya kimkakati. Hivyo Naipongeza sana Benki ya NBC kwa mafanikio haya…hongereni sana,’’ alisema Mchechu.

Aidha Bw Mchechu alitumia fursa hiyo kuwasilisha agizo la Rais Samia Suluhu unaoyaka mashirika na taasisi nyingine zenye umiliki wa umma kuhakikisha zinatimiza wajibu wao wa msingi wa kuwasilisha gawio kwa serikali.

“Anachosisitiza Mheshimiwa Rais kwenye hili ni kwa taasisi hizi kutimiza wajibu huu kwa fedha zitokanazo na faida iliyopatikana tu na si kwa taasisi hizi kukopa mahali popote ili kulipa gawio. Hata hivyo taasisi zitakazoshindwa kutimiza wajibu ipo haja ya viongozi wa taasisi hizi kujitafakari ili kuona kama kweli wanastahili kuendelea kuongoza taasisi zisizo tengeneza faida kwa taifa,’’ alisema.

Awali akizungumza kwenye tukio hilo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NBC, Dk. Elirehema Doriye, alieleza kuwa mafanikio na mwenendo chanya wa benki hiyo unathibitisha imani kubwa waliyonayo wateja kwa kwa Benki hiyo.

“Tuna furaha kusalia katika dhamira yetu ya kufikia malengo yetu muhimu katika kupanua nyayo zetu na kuwekeza katika teknolojia ili kuboresha uzoefu wa wateja wetu. Faida yetu ya kabla ya kodi ilikua kwa asilimia 36 hadi TZS 81.9 bilioni kutoka TZS 60 bilioni mwezi Desemba 2021.’’

“Ongezeko hili la faida ndilo linatuwezesha kutoa TZS 20 bilioni kama gawio kwa wanahisa wetu; leo, tunafurahi kukabidhi hundi ya TZS 6 bilioni kama gawio kwa mwaka 2022. Tunatazamia mustakabali wenye matumaini zaidi huku pia tukiwa tunaendelea kutoa huduma bora zaidi kwa wateja wetu.” Alisema Bw Doriye.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi aliishukuru Serikali kwa kuweka mazingira mazuri kwa taasisi za fedha kama Benki ya NBC kustawi huku pia akiipongeza Bodi ya wakurugenzi wa benki hiyo pamoja na wafanyakazi kwa jitihada kubwa walioifanya hadi kufikia mafanikio hayo.

“Utendaji kazi wa Benki unaonyesha mazingira bora ya biashara ambayo yalituruhusu kuwafikia wateja wetu kwa urahisi. Tutaendelea kuwekeza katika teknolojia, kupanua nyayo zetu na kuboresha huduma zetu zetu ili kukidhi na kuzidi matarajio ya wateja wetu.” Alisema Bw Sabi.

Akizungumzia uwajibikaji wa benki hiyo kwa jamii Bw Sabi alisema katika kipindi cha mwaka 2022 benki hiyo ilifanikiwa kukusanya pesa kiasi cha TZS 200M kupitia mbio za NBC Dodoma Marathon 2022 ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi.

“Benki ya NBC ndiyo mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania ‘NBC Premier League”, ambayo inazalisha ajira na kusaidia uwezeshaji na ushirikishwaji wa kifedha.’’ Aliongeza Bw Sabi huku akibainsha kuwa benki hiyo iliongeza matawi matano mapya katika kipindi cha mwaka wa 2022 huku wakala wa mtandao wa benki hiyo “NBC Wakala” ukukua kwa asilimia 82 kutoka mawakala 5,121 hadi 9,525.

Mwisho.

 

Caption

Msajili wa Hazina Bw Nehemiah Mchechu (wa tatu kushoto) akipokea mfano wa hundi yenye thamani ya Tsh 6 Bilion kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (Kushoto) ikiwa gawio la mwaka 2022 kwa Serikali ambayo inamiliki asilimia 30 ya hisa za benki hiyo. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NBC, Dk. Elirehema Doriye (wa pili kushoto) pamoja na maofisa waandamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents