NIT chatakiwa kukamilisha kwa haraka hosteli ya wanafunzi, jengo la wataalamu sekta ya anga

SERIKALI imekitaka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kukamilisha kwa haraka jengo la hosteli za wanafunzi na la kufundishia wataalamu mbalimbali katika sekta ya anga wakiwemo marubani na mafundi wa ndege ili watanzania waweze kunufaika nayo.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile wakati alipotembelea chuo hicho kwa lengo la kufanya ziara ya kukagua majengo hayo yanayoendelea kujengwa chuoni hapo.
Kihenzile amesisitiza kuwa Mkuu wa Chuo cha NIT Dk. Prosper Mgaya kuendelea kusimamia wakandarasi hao ili ujenzi wa Majengo hayo ya hosteli za wanafunzi na madarasa ya kufundishia wataalamu hao katika sekta ya anga kukamilika kwa wakati uliopangwa.
Amesema licha ya kuhakikisha majengo hayo yanakamilika kwa wakati, ni muhimu pia yakajengwa kwa ubora unaozingatiwa kwani watakaoishi na kusoma katika majengo hayo ni binadamu.
“Tukijengewa maghorofa ambayo muda mchache yataanza kutikisika hiyo itakuwa ni hatari kwa vijana wetu, ninaamini mradi huu ukikamilika utakuwa na viwango vinavyokubalika na utakwenda kunufaisha watanzania wote,” amesema na kuongeza
“Ni muhimu chuo kuwa karibu na hawa wanaosimamia mradi huu ili kuhakikisha sababu za kukwamisha mradi zinapungua, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na serikali yake wanatenga fedha nyingi ili kuboresha sekta mbailmbali ikiwemo elimu hivyo hatupaswi kumuagusha,” alisema
Aidha Naibu Waziri Kihenzile amekitaka chuo hicho kuhakikisha kinaendelea kufanikisha utoaji wa wataalamu wa kutosha watakaokwenda kuendesha na kusimamia miradi mikubwa ya serikali katika sekta ya usafiri wa anga, majini na nchi kavu.
“NIT tunawategemea na kuwatumaini katika kutengeneza wataalamu hawa ambao watakwenda kuhudumia miundombinu hii ya usafirishaji inayoendelea kujengwa nchini, hatutategemea miradi inakamilika lakini tunatafuta wataalamu kutoka nje ya nchi,” amesema
Naye Mkuu wa chuo cha NIT, Dk. Mgaya amesema chuo hicho kinatekeleza mradi ambao unafadhili ujenzi wa majengo matano ikiwemo hosteli hiyo ya wanafunzi yenye mabweni mawili ambapo kila bweni moja litachukua wanafunzi 752.
Amesema kukamilika kwa hosteli hiyo kutatatua changamoto ya maladhi ya wanafunzi 1500, huku kituo mahili cha usafiri wa anga ambacho kina majengo matatu kitaongeza ufanisi katika upatikanaji wa wataalamu.
“Tumepokea maelekezo yote ya Naibu Waziri na tunaahidi kuwa tutayafanyia kazi kwa kuhakikisha kabla ya muhula mpya wa masomo majengo haya yawe yamekamilika, na hatutamwagusha tutajitahidi majengo haya yakamilike kwa ubora unaotakiwa.
“Pia tutahakikisha tunatoa wataalamu wenye weledi na ujuzi ambao watakwenda kusimamia miradi mikubwa ya serikali ikiwemo ya reli ya kisasa ya SGR, usafiri wa maji pamoja na anga,” amesema
Written by Janeth Jovin