Nyasa walivyoadhimisha Uhuru wa Tanganyika kwa kufanya usafi hospitalini
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Peres Magiri, ameongoza viongozi wengine waandamizi wa wilaya hiyo, vikosi ya ulinzi na usalama, watumishi na wananchi wilayani humo kufanya usafi katika hospitali ya Nangombo kuadhimisha miaka 63 ya uhuru wa iliyokuwa Tanganyika.
Mkuu huyo wa wilaya alisema uamuzi huo wa kusafisha hospitali hiyo ya wilaya ulikuja kufuatia maelekezo kutoka serikalini ya kuadhimisha siku hiyo kwa shughuli za kijamii na taasisi zilizotenga fedha kwa ajili ya shughuli hiyo zielekezwe katika kusaidia na kuhudumia mahitaji mbalimbali ya jamii husika.
Kutokana na maagizo hayo kutoka serikalini, Magiri alisema: “Kwa hiyo ndio sababu sisi wilaya ya Nyasa tuliamua tutashiriki kwenye maadhimisho haya kwa kufanya usafi hapa lakini pia kwa kile ambacho tumeweza kuwa tumepata, kwa ajili kama matendo ya huruma, kuwasaidia wagonjwa waliolazwa hapa, ” alisema Magiri.
Magiri pia alitumia fursa hiyo kuwashukuru wote waliojitokeza kwenye usafi huo, hususan vikosi vya ulinzi na usalama, na kuwataka waendeleze moyo huo katika matukio mengine yatakayojitokeza siku zijazo.
Akizungumza baada ya shughuli hiyo ya usafi, Katibu wa Hospitali hiyo, Martin Ngore, alimshukuru mkuu huyo wa wilaya kwa uamuzi wake wa kuagiza siku ya uhuru wa Tanganyika iadhimishwe kwa shughuli ya usafi hospitalini hapo na akasema jambo hilo limesaidia mazingia ya utoaji tiba.
“Usafi uliofanyika unatengeneza mazingira mazuri ya kutolea huduma kwa hospitali lakini pia matendo ya huruma yaliyofanyika kwa wagonjwa wetu tunasema hii ni sehemu ya tiba,” alisema Ngore.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya Magiri ameshauri vyombo vya ulinzi na usalama wilayani Nyasa viwe na shughuli za pamoja ikiwemo mazoezi ya pamoja au hafla mbalimbali ikiwemo za kukaribisha mwaka.
Written by Angel Kayombo, Ruvuma