Nyumba zasombwa na maporomoko ya Udongo
Takriban watu 13 wameuawa katika maporomoko ya udongo mashariki mwa Uganda, lakini maafisa wanahofia kwamba idadi halisi ya waliokufa ni kubwa zaidi kwani takriban nyumba 40 zilisombwa na maji.
Maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa yaliathiri vijiji vingi katika wilaya ya Bulambuli, takriban kilomita 280 kutoka mji mkuu Kampala.
Shirika la Msalaba Mwekundu cha Uganda kimesema takriban watu 13 wamefariki, lakini AFP imeripoti kuwa idadi ya waliofariki inaweza kufikia watu 30.
Operesheni ya uokoaji inaendelea, Shirika la Msalaba Mwekundu la Uganda lilisema kwenye X.
Miili mingi iliyopatikana ni ya watoto, kulingana na gazeti la ndani la Daily Monitor. Makumi ya watu bado hawajulikani waliko.
Mvua kubwa imenyesha katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki kwa siku chache zilizopita.
Siku ya Jumatano, Ofisi ya Waziri Mkuu ilitoa onyo la maafa kupitia X.
Kingo za mito zimepasuka, shule na makanisa zimefurika na kuharibu madaraja, na kuwatenga watu wengi . Wanajeshi wametumwa kusaidia katika juhudi za utafutaji na uokoaji.