Petrol DSM sasa ni Tsh 3261 kutoka Tsh 3314

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza kushuka kwa bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa Nchini zitakazotumika kuanzia leo Jumatano June 05, 2024 saa 6:01 usiku ambapo kwa mwezi huu wa June 2024, bei za rejareja za mafuta katika Mkoa wa Dar es Salaam petrol ni Tsh. 3261 kwa lita, dizeli Tsh. 3122 na mafuta ya taa 3261.
EWURA imesema mabadiliko ya bei za mafuta kwa mwezi June 2024 yamechangiwa na kupungua kwa bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia (FOB) kwa wastani wa asilimia 11.82 kwa mafuta ya petroli, asilimia 7.77 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 7.94 kwa mafuta ya taa, kuongezeka kwa wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni (Applicable Exchange Rate) kwa 1.4%”
“Sababu nyingine ni kupungua kwa gharama za uagizaji wa mafuta (premiums) kwa wastani wa asilimia 2.06 kwa petroli na asilimia 8.51 kwa dizeli katika Bandari ya Dar es Salaam, kuongezeka kwa gharama za uagizaji wa mafuta kwa wastani wa asilimia 7.07 kwa petroli na asilimia 25.24 kwa dizeli katika Bandari ya Tanga, na zimepungua kwa wastani wa asilimia 12.64 kwa mafuta ya petroli na 12.61 kwa mafuta ya dizeli katika Bandari ya Mtwara”
Itakumbukwa bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa Nchini kwa mwezi uliopita zilizoanza kutumika kuanzia Jumatano May 01, 2024 saa 6:01 usiku, bei za rejareja za mafuta katika Mkoa wa Dar es Salaam petrol ilikuwa ni Tsh. 3314 kwa lita, dizeli Tsh. 3196 na mafuta ya taa 2840.
Imeandikwa na Mbanga B.
CC: Millard ayo.