Polisi Derek Chauvin aliyemuua George Floyd akutwa na hatia, shuhudia ilivyokuwa (+ Video)

Majaji nchini Marekani wamempata na hatia afisa wa polisi wa zamani kufuatia kifo cha Mmarekani mweusi George Floyd huko Minneapolis mwaka jana.

Derek Chauvin, 45, alinaswa katika kanda ya video akipiga goti kwenye Shingo ya Bw. Floyd kwa zaidi ya dakika tisa alipokamatwa mwezi Mei mwaka uliopita.

Video hiyo iliyotazamwa sana iliibua hisia kali na kusababisha maaandamano dhidi ya ubaguzi wa rangi kote duniani na utumiaji wa nguvu kupita kiasi unaofanywa na kikosi cha polisi.

Chauvin alipatikana na makosa matatu: mauaji ya kiwango cha pili, kiwango cha tatu na mauaji bila kukusudia.

Atasalia kizuizini hadi atakapohukumiwa na huenda akafungwa jela kwa miongo kadhaa.

Jopo la majaji 12-lilichukua chini ya siku moja kufikia uamuzi huo.

Baada ya pande zote kutoa kauli zao za mwisho siku ya Jumatatu, majaji walijitenga katika hoteli kujadili kwa makini uamuzi wao.

Walikubaliana kwa kauli moja kwamba hawarudi nyumbani hadi wafikie uamuzi wao.

Uamuzi huo ulishangiliwa kwa vifijo na nderemo nje ya mahakama, ambako mamia ya watu walikuwa wamejitokeza kufuatilia tangazo hilo.

Wakili wa familia ya Floyd, Ben Crump, alisema ni hatua ya “muhimu hatika historia” ya Marekani.

“Haki iliyopatikana kwa uchungu hatimaye imefika, aliandika katika twitter

Rais Joe Biden na makamu wake Kamala Harris waliipigia simu familia ya Floyd mara baada ya uamuzi huo.

Bw. Biden Alisikika akisema “hatimaye haki imetendeka”.

“Tutaongeza juhudi kuhakikisha mengine yanafikiwa. Hii itakuwa hatua ya kwanza muhimu ya kukabiliana na ubaguzi wa rangi uliokithiri katika mifumo yetu,” rais alisema.

Na katika hotuba ya kitaifa iliyopeperushwa kwenye runinga muda mfupi baadaye, Bwana Biden alisema: “Ubaguzi wa kimfumo ni doa kwa roho ya taifa lote.”

Rais wa Marekani Joe Biden

CHANZO CHA PICHA,EPA

Wakati huo huo, Bi Harris aliwahimiza wabunge kupitisha muswada wa George Floyd unaolenga kurekebisha idara ya polisi nchini Marekani . “Muswada huu ni sehemu ya urithi wa George Floyd. Kazi hii ni ya muda mrefu,” alisema.

Shirikisho la polisi la Minneapolis, shirika lisilo la faida linalowakilisha polisi – lilishukuru jopo la waliotoa uamuzi huo kwa “kazi yao ya kujitolea” kubeba “mzigo mkubwa”.

Shangwe katika viwanja vya Black Lives Matter Square, Washington

“Tunataka pia kufikia jamii na bado tueleze masikitiko yetu makubwa kwa maumivu yao, kwani tunayahisi kila siku pia. Hakuna washindi katika kesi hii na tunaheshimu uamuzi wa majaji,” shirikisho lilisema.

“Tunahitaji kutuliza siasa na kukomesha harakati za viongozi waliochaguliwa kukoma kuendelea kuzua uhasama kwa msingi wa rangi.”

Chauvin anatarajiwa kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo, kulingana na ripoti za vyombo vya habari nchini Marekani.

Wanasema njia moja ya uwezekano wa kukata rufaa ni utangazaji mkubwa uliotolewa kwa kesi hiyo, na timu ya utetezi ikisema kwamba hii inaweza kuwa imeathiri majaji.

Pia, Jaji aliyeongoza kesi hiyo Peter Cahill alisema Jumatatu kwamba maoni yaliyotolewa na Mwanasiasa wa Democrat Maxine Waters yanaweza kuwa sababu ya kukata rufaa.

Mwishoni mwa wiki, Bi Waters alikuwa amewataka waandamanaji “kusalia barabarani” na “kuzua malalamiko zaidi” ikiwa Chauvin ataachiliwa.

Ni nini kilichotokea kwa George Floyd?

Mwanamme huyo mwenye umri wa miaka 46 alinunua pakiti ya sigara katika duka moja huko Minneapolis Kusini jioni ya tarehe 25 Mei 2020.

Msaidizi wa duka aliamini alitumia sarafu bandia ya $ 20 na akapiga simu kwa polisi baada ya Bw Floyd kukataa kurudisha sigara.

Usalama ulikuwa umeimarishwa Minneapolis kabla ya uamuzi huo

Polisi walipofika, walimuamuru Bwana Floyd atoke kwenye gari lake lililokuwa limeegeshwa na kumfunga pingu. Makabiliano yalitokea wakati maafisa walipojaribu kumtia bwana Floyd kwenye gari la kikosi chao. Walimuangusha chini na kumkandamiza

George Floyd alikufa vipi?

Upasuaji uliofanywa kama sehemu ya uchunguzi baada ya kifo cha Bwana Floyd, haukupata ushahidi wowote wa shinikizo la kubanwa kifua au kunyongwa.

Matokeo ya uchunguzi wa daktari yameonesha kwamba Bwana Floyd alikuwa na matatizo ya moyo na mchanganyiko wa yote hayo mawili, pengine vichocheo fulani katika mfumo wake na kukandamizwa na maafisa huenda kulichangia kifo chake.

Ripoti inasema kwamba Bwana Chauvin aliweka goti lake juu ya shingo ya Bwana Floyd na kumkandamiza kwa dakika 8 na sekunde 46 – ambapo Bw.Floyd hakuamka tena.

George Floyd alipoteza maisha mwaka jaa mwezi Mei

Karibia dakika mbili kabla ya kuondoa goti lake maafisa wengine waliangalia kiganja cha mkono cha Bwana Floyd ikiwa bado mapigo ya moyo yapo lakini hawakuona chochote.

Alipelekwa katika Kituo cha Matibabu kaunti ya Hennepin kwa kutumia gari la kubeba wagonjwa na kusemekana kwamba amekufa karibu saa moja baadae.

Nini kilitokea wakati wa kesi?

Wakati wa kesi ya Chauvin, majaji walisikia kutoka kwa mashahidi 45 na kutazama saa kadhaa ya video.

Ushahidi wenye nguvu zaidi ulitoka kwa walioshuhudia tukio hilo. Watu Kadhaa waliangua kilio huku wakitazama picha za tukio hilo na kuelezea kujisikia “wanyonge” wakati matukio yakifanyika

Courteney Ross, rafiki wa kike wa Bw Floyd wa miaka mitatu, na Philonise Floyd, mdogo wake, pia waliingia kizimbani ili kutoa maelezo kumhusu mwathiriwa.

Mashahidi wataalam kwa niaba ya serikali walisema kwamba Bw Floyd alikufa kutokana na ukosefu wa oksijeni kutokana na njia ya kumzuia iliyotumiwa na Chauvin na wenzake.

Chauvin mwenyewe alichagua kutotoa ushahidi, akiomba haki yake ya kutojihukumu mwenyewe na majibu yake.

Mashtaka ni yapi?

Mauaji ya kutokusudia ni wakati mtu anaposababisha kifo cha mwingine bila kukusudia kusababisha maafa .

Katika mauaji ya daraja la pili, kitendo ambacho kilisababisha kifo cha mtu kinaweza kuwa cha kukusudia au kutokusudia. Hukumu ya juu kwa shtaka hili ni miaka 40 gerezani.

Mauaji ya kiwango cha tatu ni shtaka linalomaanisha kuwa mtu binafsi ametenda kwa njia ambayo inahatarisha mtu mmoja au zaidi, na kusababisha kifo

Uamuzi wa majaji ulipokewa kwa shangwe

Maafisa wa polisi wamehukumiwa mara chache – ikiwa wanashtakiwa kabisa – kwa vifo vinavyotokea kizuizini, na uamuzi katika jaribio hili umeonekana sana kama dalili ya jinsi mfumo wa sheria wa Marekani utakavyoshughulikia kesi kama hizo siku zijazo.

Majaji waliafikiaje uamuzi wao?

Watoa uamuzi 12 walipewa jukumu la kuamua ikiwa Chauvin atakabiliwa na kifungo gerezani au ataachiliwa huru.

Majaji wote hawakufahamika na hawakuonekana wakati wa kesi hiyo, lakini idadi kubwa ililenga vijana, wazungu zaidi na wanawake zaidi.

Baada ya pande zote mbili kuwasilisha hoja za mwisho siku ya Jumatatu jopo lilitengwa katika hoteli bila mawasiliano ya nje ili waweze kujadili uamuzi.

Walipaswa kukubaliana juu ya uamuzi wa pamoja na waliambiwa hawawezi kurudi nyumbani kabla ya kufanya uamuzi wao.

Bofya hapa chini kutazama.

https://www.instagram.com/tv/CN6z3IthqSY/

Related Articles

Back to top button