Polisi Morogoro wamsaka aliyeua na kufukia ndani

Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamtafuta Mwanaume mmoja anayedaiwa kuhusika na mauaji ya Mwanamke wake aitwae Lilian Daniel (27), Mkulima na Mkazi wa Kijiji cha Changalawa, Wilaya ya Kilosa ambaye anadaiwa kumuua na kumzika ndani ya nyumba waliyokuwa wakiishi kama Mume na Mke na kisha kumzika ndani
Taarifa za awali zimeeleza kuwa tukio hilo liligundulika tarehe 8 Machi 2026 baada ya Ndugu na Wananchi kuanza kumtafuta Lilian bila mafanikio tangu mwezi December 2025 ndipo likaja wazo la wao kuamua kufika katika nyumba ya Mtu aliyedaiwa kuwa na uhusiano naye wakihisi anaweza kuwa na taarifa kuhusu alipo.
Imeelezwa kuwa wakati wakichunguza nyumba hiyo Ndugu na baadhi ya Wananchi waligundua uwepo wa kaburi ndani ya nyumba hiyo na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ndipo ukapatikana mwili uliokuwa umefukiwa ndani.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na juhudi za kumtafuta Mtuhumiwa zinaendelea, pia wametoa wito kwa Mtu yeyote mwenye taarifa zinazoweza kusaidia kupatikana kwa Mtuhumiwa huyo ( ambaye jina lake halijatajwa ) watoe ushirikiano kwa kufika katika kituo cha Polisi kilicho karibu au kuwataarifu Viongozi wa Serikali za mitaa.




