Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam kwa kushirikiana na Timu Maalum ya Kuzuia na Kupambana na Uhalifu wa Mtandaoni, huku ikiwashirikisha Polisi Mkoa wa Morogoro, wamefanya Operesheni maalum kuanzia tarehe 18/05/2022 hadi 26/06/2022 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam na Mkoa wa Morogoro na kufanikiwa kuwakamata Julius Simon Mwabula @ Kibegi, miaka 20, Mhehe, mkazi wa Ifakara Morogoro na wenzake ishirini na mbili (22) kwa tuhuma za kufanya uhalifu kwa njia ya mtandao.
Watuhumiwa hao wamekuwa wakijifanya wao ni Wakuu wa shule, Waganga wa kienyeji, Ndugu wa wahanga, Wahudumu wa makampuni ya simu (customer care) au mawakala wa Freemason, ambapo huwatumia watu ujumbe mbalimbali kupitia namba tofauti za simu na kujifanya wanania ya kusaidia watu badala yake huishia kuwaibia ( kuwatapeli).
MFANO WA UJUMBE NI
“Halo ndugu mzazi mwanao shuleni amepatwa na matatizo na anaumwa sana hivyo tuma pesa haraka ili nimpeleke hospitali” na muhalifu huyo anatoa namba ya kutuma hiyo pesa na ukituma unakuwa umeibiwa.
Watuhumiwa hao wamekutwa wakiwa na vifaa mbalimbali ambavyo wanavitumia kufanya uhalifu huo, vifaa hivyo ni kama ifuatavyo:
1. Kompyuta mpakato (laptop) 2,
2. Kompyuta ya mezani (desk top) 1,
3. Simu za aina tofauti 28,
4. Flash 2,
5. Modem ya mitandao yote 1,
6. Kadi za simu za mitandao mbalimbali zaidi ya 50.
Written and edited by @yasiningitu