Habari

Profesa Mbarawa: Ujenzi Bandari ya Mbamba Bay umezingatia mabadiliko ya hali ya hewa kwa miaka 50 ijayo

‎Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa Ujenzi wa Bandari ya Mbamba bay umezingatia mabadiliko ya hali ya hewa kwa miaka hamsini ijayo.

‎Profesa Mbarawa, ameyasema hayo baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa Bandari hiyo, iliyopo wilaya ya Nyasa Mkoa wa Ruvuma, inayogharimu takribani billioni 80, ambapo bilioni 75.8 kwaajili ya Mkandarasi na bilioni 5 kwaajili ya usimamizi.

‎Amesema mpaka sasa ujenzi huo umefikia asilimia 47 na kwamba kwenye usanifu wa Bandari hiyo wameangalia mabadiliko ya tabia ya nchi ya miaka hamsini inayokuja.

‎“Tumeangalia miaka hiyo kwasababu unaweza kujenga Bandari leo lakini baada ya muda maji yakajaa, bandari hii tumeijenga katika kiwango ambacho hata kama kutabadilika, viwango vya maji kupanda na kushuka itafanya kazi kama ilivyotarajiwa,” amesema Profesa Mbarawa



‎Aidha Profesa Mbarawa ,ametoa wito kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Wakandarasi kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati kama walivyoahidi kwa viongozi pamoja na wananchi.

‎“Wito wangu kwa TPA tumsimamie mkandarasi, tuhakikishe kwamba huo muda ambao, tumewaahidi viongozi na wananchi, tuweze kukamilisha kabla ya wakati huo,” amesema

‎Vilevile Profesa Mbarawa, Amejibu hoja Ya Mbunge wa Nyasa John Nchimbi, Inayohusu kulipwa kwa fidia kwa Wananchi wa eneo hilo, Kwa kuwaahidi Wananchi waliokuwa wamepisha ujenzi wa bandari hiyo wataanza kulipwa mara baada ya wataalamu kuja kuhakiki.

‎“Serikali hii inawapenda sana watanzania, na kila mtu ambaye anastahili kulipwa fidia, kwa mujibu wa Sheria, tu-underline (tupigie mstari) kwa mujibu wa sheria tunawalipa na hao, tayari wananchi wa hapa wameshafanyiwa tathimini, watakuja wataalamu kuhakiki halafu tutaanza kuwalipa,” amesema

‎Akielezea mradi huo Muhandisi John Paul msimamizi wa mradi kwa upande wa TPA, amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi wa nane na tayari umeshafikia asilimia 47 ya utekelezaji wake.

‎“Ujenzi wa bandari hii ulianza Januari 26,2024, ilkuwa utekelezwe kwa kipindi cha miezi 24, lakini kwasababu za kimkataba, sanasana inshu nyingi zilikuwa ni za kiusalama, zilifanya tukachelewa kidogo, kwahiyo mkandarasi ameongezewa muda wa ziada wa miezi saba, na tunatarajia kwamba mradi huu sasa utakamilika  Agosti 26, mwaka huu (2026). Kwa sasa hivi mlivyoona mradi wetu umeshafikia asilimia 47 ya utekelezaji wake,” amesema

Written by Angel Kayombo, Ruvuma

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents